Pages

Saturday, April 19, 2014

Wapiga mabao Simba, Yanga waingia mitini


NI wazi kuwa Simba itaingia uwanjani bila ya Betram Mwombeki wala Mrundi Gilbert Kaze, na Yanga pia haitakuwa na Emmanuel Okwi ambao wote walizisaidia timu zao kupata mabao kwenye mechi mbili za mwisho za timu hizo.
 

Mwombeki na Kaze walikuwa mashujaa wa mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara baada ya kuisaidia timu hiyo kutoka nyuma na kupata sare ya mabao 3-3 kwa kuchomoa mabao mawili kati ya hayo na jingine akatupia Joseph Owino.
 

Okwi pia aliitoa Yanga kimasomaso kwenye mechi ya Mtani Jembe baada ya kuwapatia bao la kufutia machozi kwenye mchezo ulioisha kwa Yanga kufungwa mabao 3-1.
Lakini pamoja na yote hayo, wachezaji hao wanakosekana kwenye mchezo wa leo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar kutokana na matatizo mbalimbali yanayowasibu.
 

Mwombeki alikuwa akisumbuliwa na homa ya matumbo hivi karibuni kisha ikaripotiwa kuwa amepona lakini hajaonekana kwenye mazoezi ya timu hiyo mpaka leo huku akikosekana katika idadi ya wachezaji waliochaguliwa na kocha Mcroatia Zdravko Logarusic kwa ajili ya kwenda Zanzibar kuweka kambi ya maandalizi ya mechi hiyo.

Kaze naye pia hataweza kuitumikia timu hiyo katika mechi hiyo kutokana na majeraha yake ya goti yanayomsumbua na kumuandama kwa muda mrefu sasa.
 

Mpaka jana, Okwi hakuwepo kwenye kikosi kilichopo chini ya kocha Mholanzi, Hans van Der Pluijm, kinachojiandaa na mechi ya Simba ya leo kutokana na madai yaliyopo kwamba Okwi ameigomea timu hiyo mpaka amaliziwe fedha zake za usajili huku uongozi ukikana mara kadhaa kuwa hakuna madai yoyote baina ya Okwi na Yanga.

No comments:

Post a Comment