Pages

Saturday, August 23, 2014

TUNAITUMIA DIJITALI VIZURI?

Madenti mambo vipi?
Naona maisha yanaendelea na kwa sisi mashabiki wa soka la Ulaya, msimu wetu ndiyo umeshawadia. Hili soka la Bongo tunamuachia Malinzi na wapambe wake wazidi kuliporomosha, sisi macho yetu kule Premiership, La Liga, Bundesliga, Serie A, Ligue 1 na kadhalika.

Leo nina mada ambayo kwa kweli siwezi kuizungumzia kwamba eti enzi zetu. Labda tu niseme kwamba wakati ule sisi tukisoma, teknolojia hii ya sasa, ilikuwa ndiyo inaingia na kwa maana hiyo ilitupita.

Nazungumzia simu, kompyuta na zaidi mtandao wa Internet. Simu tulitumia zile za mezani, yaani hadi urudi nyumbani au uende posta ndipo unaweza kuwasiliana na mwenzako, lakini nao kwao wawe nayo.
Sasa nyinyi maanko mko kizazi cha Digitali, mnamiliki simu zenu za mkononi, tena basi teknolojia ikiwa imewawekea kila kitu, yaani simu lakini pia unaweza kupata internet inayokuingiza kwenye mitandao ya kijamii ambayo inapendwa sana na vijana kama Instagram, Twitter, Facebook, Viber, Tango, WhatsApp, YouTube na kadhalika.
Kwa kuwa sisi enzi zetu mambo haya hayakuwepo, siwezi kuweka ulinganisho na ilivyo leo, lakini uzoefu nilionao katika mitandao hii, unanifanya nijiulize kama tunaitumia kwa faida ya maisha yetu ya baadaye au tunafanya ili kujifurahisha tu.
Internet ina faida nyingi sana kwenu, kwa sababu unaweza kujifunza vitu vingi kama utapata mwongozo wa mwalimu kuhusu kitu chochote duniani. Sisi tulio ofisini inatusaidia sana kupata taarifa za sasa hivi zinazotokea popote. Hatupishani tena na habari kama ilivyokuwa zamani tulipolazimika kusubiri magazeti ya siku hiyo ndiyo tujue kilichotokea juzi.
Kule kwenye hiyo mitandao ya kijamii, vijana ni wengi na bila shaka wanafunzi pia mpo wa kutosha. Ninaona baadhi yao wanatupia picha wakionekana wapo bize kimasomo, ingawa inasikitisha kuona pia wengine ni kama wanajiuza flan, kwa kuanika picha zao walizopiga wakiwa nje kabisa ya mstari wa maadili.
Acha hiyo ya kujianika, lakini pia lingine linalokera ni jinsi wanavyopigana vikumbo kutafuta marafiki wenye majina makubwa. Kila mtu anataka kuwa friends na Diamond, Dimpoz, Wema, Kajala, Masanja Mkandamizaji, Kidoti, Ray na mastaa wengine kemkem.
Sikatai, ni jambo zuri kuchat na marafiki, hasa kama hawa mastaa wetu, lakini najiuliza kama hili ndilo jambo pekee tunalolifanya kupitia mitandao hii. Maana kutwa utakuta madenti wanasimuliana jinsi Chris Brown alivyomnanga Rihanna katika akaunti yake ya Twitter!
Siku hizi kuna hadi kutumiana picha kupitia simu zetu za mikononi, wenyewe mnaita WhatsApp. Utawasikia, simu yako ina wazap? Nataka nikutumie bonge la picha nipo beach jana nakula bata!
Nijaribu tu kuwashauri madenti ambao kwa vyovyote nyinyi ni baba na mama watarajiwa, kwamba huu ni wakati mzuri sana wa kujaribu kutengeneza maisha yetu ya kesho kupitia mitandao, hasa kwa mambo yanayohusu masomo.
Zamani sisi tulikuwa tunasoma kitabu kimoja kiliitwa Jiandae, chenye maswali mengi ya kila masomo tunayosoma. Sijui kama kipo siku hizi. Kitabu hiki kilikuwa kinakusanya mitihani mingi ya taifa ya darasa la saba iliyofanywa miaka ya nyuma yake, ili kumwandaa mwanafunzi kwa mtihani wake wa kumaliza elimu ya msingi.
Lakini ninavyojua mimi, hivi sasa unaweza kujifunza au kupata mitihani ya kidato cha nne ya mwaka jana kupitia internet. Ukajifua na kujifua kuusubiri mtihani wako wa kidato cha nne au sita.
Ni bahati mbaya tu kwamba muda ukipita huwa haurudi, lakini nataka niwaapie kuwa kama ndiyo ningekuwa denti sasa hivi kwa akili hizi na teknolojia hii, mngenikamatia pale kwenye kile kibao cha HAKUNA SHULE MBELE!

No comments:

Post a Comment