Pages
▼
Saturday, November 1, 2014
Kiemba, Chanongo waongezewa Adhabu
Na Nicodemus Jonas
LILE sakata la kusimamishwa kwa wachezaji watatu wa Simba, Amri Kiemba, Haruna Chanongo na Shabani Kisiga, limechukua sura mpya baada ya nyota hao kugomea agizo la rais wa timu hiyo, Evans Aveva la kuwataka kufika ofisini kwake kujieleza.
Nyota hao walisimamishwa Jumapili iliyopita baada ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons kwa utovu wa nidhamu na walitakiwa kujieleza jana kwa rais, hata hivyo hakuna aliyefika, hivyo wataendelea na kifungo hadi watakapoitwa tena.
Adhabu yao ilikuwa imalizike jana kwenye kikao na Aveva lakini hawakutokea, hivyo sasa adhabu hiyo itaongezeka kwa kuwa viongozi watasubiri mechi ya leo na Mtibwa ipite na ndipo watakaa na kupanga tarehe nyingine.Hiyo sasa inamaanisha kuwa adhabu yao itaongezeka mpaka pale uongozi utakapofanya maamuzi mengine juu ya sakata hilo.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Katibu Mkuu wa Simba, Stephen Ally, alisema nyota hao walitakiwa kukutana na rais saa tatu asubuhi kwa ajili ya kujieleza lakini hakuna aliyejitokeza, licha ya rais kuwasubiri kwa muda mrefu ofisini kwake.
Aliongeza kuwa licha ya kushindwa kufika ofisini, Kisiga peke yake ndiye alipiga simu kuwaambia kuwa alikwama kwenye foleni huku Chanongo na Kiemba wakiwa kimya.
“Waliambiwa wafike ofisini kwa rais leo (jana) asubuhi saa 3:00, lakini hakuna hata mmoja aliyetokea mpaka saa 4:30, zaidi ya Kisiga kupiga simu kutuambia kuwa alikwama kwenye foleni. Hao wengine hakuna aliyetoa taarifa kuhusu kutokuja kwao.
“Kwa hiyo rais ameamua kuendelea na shughuli zake nyingine, ikizingatiwa tupo kwenye maandalizi ya mchezo wa kesho (leo, dhidi ya Mtibwa),” alisema na kuongeza kuwa, baada ya mechi watapanga tarehe ya kuwaita tena.
Wakati huohuo, kocha Patrick Phiri, amesema kuwa licha ya Chanongo kuwa kwenye kikosi cha kwanza, haoni pengo lake kwani kuna nyota wengi wanaoweza kuziba nafasi yake.
No comments:
Post a Comment