Stori Dustan Shekidele, Morogoro/Ijumaa
MSHIRIKI
wa Shindano la Miss Tanzania mwaka 2014, aliyeshinda taji hilo katika
Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na baadaye kuthibitika kuwa
alighushi umri na hivyo kulitema na kusababisha kufungiwa kwa shindano
hilo, Sitti Mtemvu, juzikati alipokewa kama mfalme alipofanya ziara fupi
mjini Morogoro.
Mrembo huyo ambaye hivi sasa anaongoza taasisi yake inayofahamika
kama Sitti Tanzania 2015, alipofika mjini hapa, baadhi ya mashabiki wake
walijipanga kutokea eneo la Nanenane na kuambatana naye hadi katika
hospitali ya mkoa ambako alitoa msaada wa vyandarua katika wodi ya
wazazi.
Baada ya kukabidhi misaada hiyo, mrembo huyo ambaye baba yake mzazi
ni Mbunge wa Jimbo la Temeke, alikwenda hadi ofisi za Chama cha soka
mkoani hapa na kutoa msaada wa mipira mitano na seti moja ya jezi kwa
lengo la kusaidia kuimarisha michezo.
“Najisikia vizuri sana nimepokelewa kama mfalme, kundi la wananachi
wa Morogoro walijipanga maeneo ya Nanenane ambapo walinipokea, binafsi
sikutarajia kukutana na mapokezi kama haya, mimi ni Mluguru na nimekuja
kwetu Morogoro kuwasaidia watu wenye uhitaji mbalimbali,” alisema binti
huyo baada ya kumaliza shughuli zake.
Lakini katika hali ya kushangaza, alipoulizwa kuhusu anavyojisikia
baada ya kulitema Taji la Miss Tanzania, Sitti alijibu kwa mkato;
“Sijisikii vibaya na wala sitaki kuzungumza ishu ya Miss Tanzania,”
alisema na kukatisha mahojiano hayo hapohapo kabla ya kuingia kwenye
gari lake bila hata kumuaga mwandishi.
No comments:
Post a Comment