Stori: Chande Abdallah na Haruni Sanchawa/Uwazi
DUNIA
imekwisha! Binti mmoja mwenye umri wa miaka 19, Rukia Ally anadaiwa
kumuua kwa kumchoma kisu kaka yake wa kuzaliwa, Said Ally wote wakati
whga Tegeta Mivumoni, Kata ya Wazo jijini Dar es Salaam, kwa kile
kinachodaiwa kuwa ni kutokana na kijana huyo kutaka kudhibiti tabia
zisizofaa za dada yake huyo, tukio lililotokea usiku wa Januari 24 mwaka
huu.
Kwa mujibu wa habari kutoka eneo la tukio, inadaiwa kuwa binti huyo
alikuwa na kawaida ya kuondoka nyumbani kwao na kwenda kusikojulikana
ambako wakati mwingine alikuwa akikaa zaidi ya siku tatu pasipo kurejea
nyumbani, huku akiwa hana maelezo ya kutosha.
Inadaiwa kuwa siku hiyo, msichana huyo hakuwa amerudi nyumbani kwa
siku tatu, hivyo aliporejea saa tatu usiku, kaka yake alimuuliza
alikokuwa, lakini badala ya kumjibu, alimuomba aingie kwanza ndani kwake
na kuwa atarejea ili kumpatia majibu.
Aliporejea na kuulizwa swali hilo na kushindwa kutoa majibu ya
kueleweka, kaka huyo alimchapa na fimbo mguuni kama ishara ya kumkanya,
lakini inadaiwa Rukia alichomoa kisu alichokuwa amekificha nguoni mwake
na kumchoma nacho upande wa kushoto wa kifua chake.
Mama wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma, alisema binti
yake alikuwa na tabia zilizowakwaza ndugu zake, kama kuvaa nguo fupi na
kuondoka nyumbani bila kuaga.
“Kwa sababu mdogo mtu hakuwa msikivu kwa kaka yake, ndipo kaka mtu
akachukua bakora na kumchapa nayo mguuni kwa lengo la kumkanya, ndipo
ghafla nikashangaa kumuona Rukia akimchoma kisu kaka yake kifuani na
kukichomoa kisha akakimbia na kukitupa kwenye majani.
“Kauli aliyoitoa kaka yake ni kwamba: Mdogo wangu unaniua! Akadondoka
hapohapo, nikamkimbilia na kumpakata miguuni mwangu damu zikimtoka
mpaka anakata roho nilikuwa nikimtazama,” alisema mama huyo.
Aidha shangazi wa marehemu, Mariam Saidi alidai baada ya Rukia
kukimbia, alizungumza naye kwa simu lakini baadaye hakupatikana
tena.“Alinipigia nikaongea naye, akasema nimwambie mama yake awadanganye
polisi kuwa yeye hakumuua kaka yake, bali alivamiwa na majambazi,
nilipomuuliza yupo wapi nikamchukue alisema yupo Ubungo halafu
hakupatikana tena,” alisema Mariam.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mivumoni, Deodatus Kamugisha
alisema binti huyo alikuwa na tabia ya kutembea usiku na kuvaa nguo fupi
kwani kuna siku alikutana naye usiku wa manane akiwa na rafiki yake
wakitokea kwenye klabu moja ya usiku.
Taarifa zilizoifikia gazeti hili kutoka kwa mwenyekiti huyo zilidai
kuwa Rukia alikamatwa Mkuranga jioni ya Januari 24 akiwa anaelekea
mafichoni na amefikishwa kituo cha polisi Wazo Hill kwa ajili ya hatua
za kisheria huku mazishi yakifanyika siku hiyo hiyo.
No comments:
Post a Comment