MASIKINI! Staa mkali wa filamu za Kibongo, Kajala Masanja hivi
karibuni amejikuta akiwa katika wakati mgumu na wa hatari kufuatia watu
wasiojulikana kuvamia nyumbani kwake na kutoa onyo kwamba wanampa siku
tano tu za kuishi, Amani lina mkasa kamili.Ishu hiyo ya kushtusha
ilitokea usiku wa saa nane ya kuamkia juzi, Jumanne nyumbani kwa staa
huyo, Sinza Mori jijini Dar es Salaam.
WALIKUWA KWENYE TOYOTA RAV 4
Kwa mujibu wa chanzo chetu, watu hao
wapatao watatu walitinga nyumbani hapo usiku huo mnene huku wakiwa
ndani ya gari aina ya Toyota Rav 4 milango mitano rangi ya bluu ya kuiva
na kumkuta mlinzi getini ambaye yupo kwa ajili ya kulinda usalama wa
msanii huyo mwenye maadui kila kukicha.“Walikuwa watano, walikuwa kwenye
Rav 4 milango mitano, rangi ya blue ya kuiva. Wakamkuta mlinzi,
walimuuliza kama Kajala yupo, mlinzi aliwadanganya kwamba hayupo.”
MLINZI ALIJUA NI BWANA WA KAJALA
“Lakini mlinzi alidanganya
akijua mmoja wa watu hao pengine ni bwana wa Kajala kwa hiyo ili kuua
soo akasema hayupo lakini ukweli Kajala alikuwepo ndani. Yeye aliwaambia
Kajala alikwenda kumsalimia mama yake, hajarudi.
WAACHA UJUMBE MZITO
“Ndipo mmoja wao akamwambia mlinzi kwamba,
wao walikuwa na shida na Kajala lakini kwa sababu hayupo, wanaacha
ujumbe apewe haraka sana. “Walisema akirudi aambiwe kuna watu walifika,
wamempa siku tano za kuishi na kwamba wao wametumwa na mtu wa karibu na
Kajala, lakini hawakumtaja kwa jina.
“Yaani mlinzi alitumia akili
sana na kuwaambia Kajala hakuwepo ndani, alikwenda nyumbani kwao, ndiyo
ilikuwa salama yake,” kilisema chanzo hicho.
AMANI LAMSAKA KAJALA
Baada ya kuinyaka nyeti hiyo, Amani lilimsaka staa huyo na kumuuliza kama kuna ukweli wa madai hayo.
Awali, Kajala aligoma katakata kukubali akisema hajui lolote lakini
alipobanwa zaidi na kuambiwa mlinzi wake ndiye aliyenyetisha habari
hiyo, alikiri.
MSIKIE MWENYEWE
“Any way, ni kweli ishu imetokea usiku, lakini
siyo saa nane, ilikuwa kama saa sita hivi. Mimi nilikuwa nimelala,
nikaona simu yangu ikiita. Nilipoangalia ni mlinzi, nikapokea.
Akaniambia kuna watu wamekuja, wamemwambia wametumwa waniletee ujumbe
kwamba nimepewa siku tano za kuishi na wametumwa na mtu wangu wa karibu.
“Mimi sikuogopa, nilitoka hadi kwa mlinzi, lakini nilikuta gari
imeshaishia zake. Kifupi ni kwamba katika watu si waoga ni mimi, unajua
kwa nini? Naishi kwa kumtegemea Mungu sana. “Kwa hiyo siogopi japokuwa
habari hizo zimenichanganya kupita kiasi, najiuliza ni mtu wangu gani wa
karibu. Basi si mtu wa karibu bali ni adui yangu. Hivi hapa najiandaa
kwenda Kituo cha Polisi Kijitonyama (Dar) kutoa taarifa kwa ajili ya
tahadhari,” alisema Kajala.
Akaongeza: “Unajua wiki yote iliyopita nilikuwa kwenye harakati za
kumalizia filamu yangu ya Pishu. Kwa hiyo hata usiku wa jana nilichelewa
kurudi, ile naingia tu nadhani ndani ya nusu saa ndiyo watu hao
walikuja, kama ningechelewa zaidi huenda ningekutana nao getini.”
ANAMHISI NANI?
AMANI: “Kajala wewe unajijua, unadhani nani anaweza kukutumia ujumbe kama huu miongoni mwa watu wako wa karibu?”
KAJALA: “Mh! Siwezi kumtaja hata kama kichwani yupo au wapo! Nitabaki
kuwa na hisia zangu tu kwa sababu sina ushahidi. Ila kama ningewaona
kwa sura hao watu na kuwatambua huenda ningeunganisha.”
Amani: “Huna mtu ambaye hivi karibuni mmetupiana maneno mabaya kwenye simu au laivu?”
Kajala: “Sina. Mimi nipo na watu wangu ni amani tu na ndiyo maana nachangayikiwa.”
Mpaka tunakwenda mitamboni, Kajala alisema ndiyo amewasili kwenye kituo hicho polisi akisubiri kusikilizwa.
CHANZO: GPL
No comments:
Post a Comment