KUFUATIA kuibuka kwa habari ya msanii nguli,
Blandina Chagula ‘Johari’ kubeba mimba na kujifungua kwa siri hadi mtoto
kufikisha umri wa miezi 7 na kuripotiwa kwa mara ya kwanza na gazeti
‘tumbo moja’ la hili la Risasi Jumamosi, mambo mengi mapya ikiwemo
maswali yameibuka na kuzua ‘sintofahamu’ juu ya uhalisia wa jambo hilo,
Amani linakupa mchapo kamili.
Saa chache baada ya habari hiyo kusomwa na mamilioni ya Watanzania
wakiwemo wadau wa sanaa na burudani wiki iliyopita, minong’ono na
mishangao ilianza kutambaa ambapo wengi walidadisi kwa kina ili kujua
‘lipi ni tui la nazi na yapi ni maziwa’ juu ya habari hiyo.
MASWALI YALIYOIBULIWA
Miongoni mwa maswali yaliyoibuliwa ni
pamoja na mimba aliibeba akiwa wapi? Alitoka Dar kwenda Shinyanga
anakodai kujifungulia mimba ikiwa na muda gani? Anaweza kuianika kadi ya
kliniki? Nini sababu ya kuficha mimba hadi mtoto anafikisha miezi 7 na
nini kimemsukuma kumwanika mtoto?
“Jamani, mbona hatuelewi haya mambo? Hivi inawezekana kweli kwa mtu
maarufu kama Johari kubeba mimba na hadi kujifungua na mtoto kufikisha
miezi yote hiyo (7) bila kujulikana?” alihoji Latifa Lusengi wa Sinza-
Makaburini.
“Hiyo mimba aliibebea wapi? Mbona alikuwa akionekana hana tumbo?” alihoji mama Jane wa Mwananyamala.
MASTAA SASA
Kuashiria kuwa mjadala ulikuwa mzito, hoja na maswali
hayakuishia kwa wadau tu kwani hata baadhi ya mastaa waliozungumza na
mwandishi wetu ama ana kwa ana au kwa njia ya simu kwa nyakati tofauti,
walionesha wasiwasi mkubwa juu ya habari ya utata huo huku wengine
wakiomba hifadhi za nomino zao kwa kile walichokiita ni “kujitunzia
heshima kwa Johari.”
MAINDA
Ruth Suka ‘Mainda’ ndiye alifungua pazia la majadala huu
kwa upande wa mastaa, baada ya mwandishi wetu kumpigia simu na kumtaka
atoe maoni yake juu ya kujifungua kwa ‘mbia’ wake huyo.“Mmh! Kama kweli
Johari amejifungua, basi mimi nampongeza kwani kuzaa ni baraka, lakini
sasa afikirie na suala la kufunga ndoa na huyo aliyezaa naye kwani hata
umri unamruhusu, asikomee tu mtoto.”
“Nyie acheni utani bwana, sisi tunashinda naye kila siku iwe baa au
sehemu tofauti, mbona hatukuona hata hizo dalili na ishara za mimba na
sisi wanawake tunajuana sana kwa mambo kama hayo? Sijui lakini,”
alihoji msanii mwingine wa kike ambaye amekuwa akionekana mara kwa mara
na Johari na kuomba hifadhi ya jina.
“Kama ni kweli kulikoni afiche mimba?” aliuliza kwa kifupi msanii wa kiume.
JOHARI AZIDI KUPIGILIA MSUMARI
Baada ya mwanahabari wetu kusikia
maswali hayo kutoka kwa wadau na baadhi ya wasanii, alimtafuta Johari
kupitia simu yake ya kiganjani ambapo alifunguka, kisha kukata simu.
“Mimba niliibebea tumboni, kwani kwa mwanamke kuzaa ni tatizo? Au
walitaka niutangazie ulimwengu kuwa nimebeba mimba na nitajifungua siku
fulani? Siko hivyo bwana.“Wanaotangaza hadi siku za kubeba mimba ni wao
na umaarufu wao, mimi ni mtu mzima, naomba nilale kwanza, nina usingizi
sana nitakutafuta baadaye,” alisema Johari na kukata simu na kuizima
kabisa.
KUTOKA AMANI
Kuzaa ni jambo la heri, tunamuomba Johari kukata kiu
ya maswali yote ya wadau na mashabiki wake ili kuondoa mkanganyiko,
ikiwezekana aanike cheti cha mtoto ili kuwakata ‘vilimi’ wale ambao
hawataki kuamini kile anachokizungumza. Hakuna sababu ya kufanya jambo
lenye baraka na neema kama hili kuwa siri na kuficha wakati yeye ni mtu
maarufu–Mhariri.
No comments:
Post a Comment