Pages

Thursday, July 16, 2015

KINGUNGE: MCHAKATO WA KUMPATA MGOMBEA URAIS CCM ULIKUWA BATILI

Mzee Kingunge akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana.

KADA mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale Mwiru, amekosoa mchakato uliotumika kumpata mgombea urais wa chama hicho, akieleza kuwa ulifinyangwa na hivyo ni batili, haukubaliki na hauvumiliki.

Aidha, ameshauri kuwa ili chama hicho kiendelee na kampeni za uchaguzi kikiwa kimoja, ni lazima kasoro zilizotokea Dodoma zijadiliwe kwa kina kumaliza tofauti zinazoonekana kujitokeza na kupata maridhiano.

Jumapili iliyopita CCM ilimteua Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuwa mgombea wake wa urais na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea mwenza.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, Kingunge alisema viongozi waandamizi wa CCM wamekiuka kwa makusudi katiba, kanuni na taratibu za chama kuanzia kwenye vikao vya Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CC) hadi Halmashauri Kuu (Nec).

Hata hivyo, alisema maamuzi ya Mkutano Mkuu uliompitisha Dk. Magufuli anayaheshimu kwa kuwa kasoro zilijitokeza CC na Nec.

Alisema Katiba ya CCM pamoja na mambo mengine, inaeleza kuwa Kamati ya Maadili ambayo ameeleza ni kitengo ndani ya chama ina jukumu la kuandaa taarifa kuhusu wagombea na siyo kukata majina.

Alisema taarifa inayoandaliwa na kitengo hicho hupelekwa CC, ambayo kazi yake ni kumsikiliza mgombea mmoja mmoja na kumuuliza maswali yasiyopungua matatu, kisha wajumbe hukaa na kupendekeza majina matano ambayo yanapelekwa Nec.

“Kwa utaratibu wa kikatiba, sekretarieti kazi yake ni kuhudumia CC na Nec kwa kukusanya majina ya watu walioomba, inayapanga vizuri, ikikamilika inawasilisha taarifa yake kwenye Kamati Kuu…sekretarieti si kikao cha maamuzi wala si kikao cha mapendekezo, kwa hiyo mchakato hasa unatakiwa uanze kwenye Kamati Kuu,” alisema.

Kingunge alisema utaratibu ambao umetumika tangu mwaka 1995, kila mgombea atapaswa kuhojiwa na kamati kuu mmoja mmoja na kuulizwa maswali yasiyopungua matatu na kisha wajumbe huwajadili na kutoa mapendekezo ya majina matano kwenda Nec.
“Inaelekea kazi ya kupata wagombea watano ilifanywa na kitengo kinachoitwa Kamati ya Maadili na Kamati Kuu ikafikishiwa majina matano tu, kitendo hicho cha kuinyang’anya Kamati Kuu kazi yake si cha kawaida, ni uvunjifu wa taratibu na hakuna uadilifu ndani yake. Kamati ya Maadili yenyewe inavunja maadili,” alisema.

Kingunge ambaye aliwahi kushika nyadhifa kadhaa ndani ya CCM na serikalini, alisema maadili ya chama yanaanzia kwenye kuheshimu muundo wa chama, sera na taratibu zake; hivyo ukiukwaji uliofanyika Dodoma ni kukinyonga chama hicho.

Alisema inasikitisha kwamba hata baada ya kupelekewa majina matano, CC ilifanya maamuzi yake bila kuwaona wagombea wote 38 waliorudisha fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais na hata wagombea waliokatwa hawakuitwa kwenye hicho kitengo cha maadili badala yake walihukumiwa bila kusikilizwa.

“Kwa hiyo kuna mahala fulani watu wachache wamekaa wakatengeneza orodha yao na wakataka Kamati Kuu imeze. Kilichofanyika si jambo dogo tu…Mzee Abeid Aman Karume alisema nchi hii ni yetu wote na mimi nasema maana yake tunaowapa madaraka wasifike mahali wakafikiria nchi hii ni yao wao, yale madaraka ni dhamana tu; na kwenye chama ni hivyo hivyo, CCM ni mali ya wanachama wote,” alisema.

Kingunge alisema chama hicho kilitoa fomu kwa wanachama ambao waliingia gharama kuzunguka mikoa mbalimbali kusaka wadhamini lakini katika hali ya kushangaza, kitengo cha maadili kiliwapuuza na kufanya maamuzi batili.

Alisema kwa utaratibu wa chama, CC ilitakiwa kuwasilikiliza wagombea wote 38 waliorudisha fomu, kuwajadili na kutoka na mapendekezo ya majina matano kupeleka Nec; utaratibu ambao ulikiukwa.

Alisema vikao vya vyombo mbalimbali ndani ya chama vimewekwa ili kutenda haki kwa wanachama wote hivyo ni muhimu kuviheshimu kwa nia ya kuleta usawa na kwamba kilichotokea Dodoma ni dharau kwa wagombea waliochukua fomu na wanachama wote wa CCM.

“Bahati mbaya katika nchi yetu wananchi ni wavumilivu mno kiasi kwamba tumefanya wakubwa zetu tunaowapa madaraka wanajua wanaweza kufanya chochote kwa sababu hakutakuwa na chochote. Sasa mimi nasema hakutakuwa na chochote sawa, lakini hata kusema?. Kwa hiyo mimi nasema kwa niaba ya wengi walio kimya,” alisema.

Kingunge aliongeza kuwa: “Na mpaka hapo kwenye CC yaliyofanyika si sahihi na kwa kweli ni batili. Upande mmoja Kamati Kuu kunyang’anywa kazi yake na kitengo lakini upande mwingine haki ya asili ya kusikilizwa, watu hawawezi kuhukumiwa tu bila kusikilizwa. Kamati Kuu inatakiwa iandae orodha fupi ya hao walioomba lakini baada ya kuwasikiliza.”

Hata hivyo, alisema Nec ina mamlaka ya kuhoji mapendekezo ya CC, kuyakubali, kukataa baadhi au yote; lakini katika hali ya kushangaza, haikufanyika hivyo.

Alisema mjadala kwenye Nec ulivyokuwa hata wazee wastaafu ndani ya CCM ambao ni marais wastaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Amani Abeid Karume, walipotoshwa na hivyo michango yao iliminya haki za baadhi ya wagombea.

Hata hivyo, alisema pamoja na upotoshaji uliofanywa na kikundi cha viongozi wachache, msimamo wa Nec ulikuwa dhahiri kwamba wajumbe walimtaka mgombea aliyekuwa na nguvu kuliko wengine, Edward Lowassa.

Bila kuwataja viongozi wakuu wa chama hicho na serikali ambao walifinyanga majina ya wagombea watano na kuyawasilisha CC, Kingunge alisema viongozi hao walifanya jitihada na nguvu kubwa kuvunja kanuni na taratibu ili kuhakikisha wanamnyima haki Lowassa.

“Kama tusipofanya critical analysis (uchambuzi kosoa), kuonyesha mapungufu yaliyojitokeza hatima ya chama chetu haitakuwa nzuri…mkasa uliotokea Dodoma ni uongozi wa chama chetu ambao vile vile ni uongozi wa nchi kutumia nguvu kubwa kabisa ya kupuuza wananchi wanasema nini na kuhakikisha kuwa huyo ambaye wananchi wanasema wanampenda, hawatampata,” alisema.

“Jitihada zote zilizofanywa za kuvunja taratibu zilikuwa zinaelekezwa kumzuia mtu fulani asipate haki na mtu huyo ni Lowassa,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Yaliyotokea Dodoma mwaka huu yametia kasoro kubwa katika historia ya chama chetu ambacho kinaheshimika sana.”

“Mkitaka nchi itengamae, lazima chama kinachoongoza kijiendeshe kwa misingi iliyosahihi na safi. Msingi wa kwanza ni demokrasia ndani ya chama. Yaliyotokea Dodoma yametia dosari kabisa kwa sababu huwezi ukabadilisha taratibu za msingi katika kupata viongozi ambazo zilipaswa kulindwa na viongozi wa chama.”

Kingunge alidai mchakato wa kumpata mgombea wa CCM ulivurugwa kwa makusudi, hivyo mkutano mkuu siyo kikao cha kulaumiwa kwa kuwa waliokosea ni CC na Nec.

“Mkutano mkuu huwezi kuulaumu kwa sababu wamepelekewa majina matatu na wametamka yule wanayemtaka…uchambuzi wangu kosoa hapa haumhusu Magufuli kwa sababu si yeye aliyefinyangafinyanga mambo,” alisema.

NINI KIFANYIKE
Alisema kutokana na kasoro hizo, ni lazima CCM ijitathimini namna ya kutoka hapo ilipo ili iweze kushinda kwa kishindo Oktoba 25 kwenye uchaguzi mkuu.

“Sisi wana-CCM tutafute njia ya kushikamana na katika hili Lowassa ana nafasi muhimu na ya kimkakati; ana imani ya mamilioni ya Watanzania. Tukitaka kufanikiwa vizuri kama CCM, tutumie nguvu zote tulizonazo twende kwenye uchaguzi tushinde kwa kishindo. Lazima yaliyotokea yazungumzwe ndani ya chama,” alisema.

Alisema bila kufanya hivyo, CCM haitaweza kuendelea kuwa moja kama ilivyokuwa awali.

“Lazima tutoke katika mazingira haya na hatuwezi kutoka hapa bila watu kutoa dukuduku zao,” alisema.

Alisema ni dhahiri kuwa ndani ya CCM kuna mvutano ambao ukiachwa utasababisha mpasuko mkubwa.

UFISADI WA LOWASSA
Alisema tangu mwaka 2008 baada ya kashfa ya Richmond, Lowassa amekuwa akiandamwa kuwa ni fisadi lakini ni ‘hadithi’ ambayo imekosa mashiko kwa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilichunguza na kuthibitisha kuwa hakukuwa na vitendo vyovyote vya rushwa.

Alisema Lowassa alilazimika kuwajibika kisiasa kwa maslahi ya CCM na serikali na kwamba siyo wa kwanza kujiuzulu kwani mwaka 1976 Mzee Mwinyi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alijiuzulu baada ya vyombo vya usalama kuthibitika kuchochea mauaji na kuumiza watu.

UADILIFU WA LOWASSA
Alisema Lowassa ni mwanachama mwaminifu wa CCM, mtendaji hodari kwenye chama na serikalini ambaye amepigiwa mfano katika kila wadhifa alioshika.

Alisema Lowassa ni kada anayependwa na wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla hivyo kumwengua kimizengwe ni udhaifu mkubwa ulioonyeshwa na viongozi wa chama hicho.

KUONDOKA CCM
Hata hivyo, Kingunge alipotakiwa kueleza imani yake ndani ya CCM na kama ataondoka, hakuweka bayana badala yake alisema atakapofikia uamuzi wa kutoka atawataarifu waandishi wa habari.

Kuhusu hatima ya kisiasa ya Lowassa, alisema ana amini ni kiongozi makini hivyo atafanya maamuzi sahihi kwa manufaa yake.

NIPASHE iliwatafuta viongozi wa CCM akiwamo Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kujibu tuhuma hizo lakini simu zao ziliita bila majibu na nyingine hazikupatikana.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment