Pages

Thursday, June 28, 2012

PICHA: MAPOKEZI YA DR. ULIMBOKA HOSPITALI YA MUHIMBILI

Wauguzi na Madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wakilisukuma gari la wagonjwa lililombeba mpigania haki zao Dk. Ulimboka wakati akitolewa chumba cha X-ray akipelekwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).



Madaktari wakisaidia kumuingiza Dk.Ulimboka katika gari la wagonjwa namba T 151 AVD la Hospitali ya AAR.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba (katikati), akizungumza na waandishi wa habari Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakati akitoa taarifa ya kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayoratibu mgomo wa madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, Dar es Salaam jana.
Dk. Cathbert Mchalo wa Taasisi ya Mifupa ya Moi (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumpokea, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania kwa ajili ya kupatiwa matibabu kufuatia majeraha aliyopata kutokana na kipigo.
Ofisa wa Polisi akimzuia mpiga picha wa gazeti la Tanzania Daima, Francis Dande, asimpige picha wakati wakimuondoa askari mwenzao aliyeshambuliwa na madaktari akituhumiwa kukutwa akipiga simu ya kuwataarifu wenzake kuwa Dk. Ulimboka hakufa.

Mmoja wa wana usalama wa (wa pili ushoto), akizozana na madaktari baada ya kumbaini akijifanya ni mwandishi wa habari na kumuamuru kuondoka eneo hilo mara moja.
Mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), wa pili kulia, akizozana na Askari Polisi waliofika hospitalini hapo wakidai wanatafuta redio yao ya mawasiliano iliyopotea wakati wa pilikapilika za kumpokea Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayoongoza mgomo wa madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, alipoletwa akiwa hoi kutokana na kipigo kutoka kwa watu waliomteka usiku wa kuamkia jana na kumtupa msitu wa Mabwepande.
Madaktari wakiwa wamepigwa butwaa nje ya viwanja vya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuatia tukio hilo.

Wauguzi wakiwa nje ya wodi ya Kibasila wakitafakari jambo kufuatia jambo hilo
Wauguzi wakiwa nje ya wodi ya Kibasila wakitafakari jambo kufuatia jambo
             Vilio vyatawala

Vilio vilitawala miongoni mwa Madaktari na Wauguzi katika Hospitali hiyo wakati Dkt. Ulimboka alipofikishwa kwa matibabu.

Madaktari walionekana wakiwa katika vikundi vikundi, huku wengine wakilaani kitendo alichofanyiwa Dkt. Ulimboka.

Wakati gari la wagonjwa likimtoa Dkt. Ulimboka kutoka katika chumba cha vipimo kwenda wodini, Madaktari waliokuwapo eneo hilo walionekana wakilisukuma gari hilo huku wakiimba mwimbo wa mshikamano, na wengine wakibugujikwa machozi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Hellen Kijo Bisimba alisema amesikitishwa sana na tukio hilo na unyama aliofanyiwa Dkt. Ulimboka.

"Serikali baada ya kuona imeshindwa kufikia muafaka na madaktari hasa baada ya kwenda mahakamani wameanza kuwatisha madaktari hao kwa kuwashambulia hii ni hatari sana kwa taifa na kitendo alichofanyiwa Ulimboka ni vitisho hatutaweza kukaa kimya kwa jambo hili," alisema Dkt. Kijo-Bisimba.


"? Usalama wa Taifa ?"

Hata hivyo, katika tukio la kumpokea Dkt. Ulimboka waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali hasa wapiga picha walikuwa na wakati mgumu kufuatia vijana wanaodaiwa kuwa ni wa  "Usalama wa Taifa" kuwazuia wasipige picha huku wakitaka kuzivunja kamera zao jambo ambalo lililalamikiwa na baadhi ya Madaktari waliohoji, ni kwa nini wawazuie wanahabari.

"Kwanini wanawazuia waandishi wa habari kupiga picha?  Waachwe wapige ili wapeleke ujumbe kwa Watanzania juu ya unyama aliofanyiwa mwenzetu," alisema mmoja wa Madaktari hao.

Waandishi wa habari walilaani kitendo cha kuzuia kufanya kazi yao na wana usalama hao.
 
Kauli ya Kamanda Kova
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, amesema Dkt. Ulimboka aliokotwa na msamaria mwema ambaye hakutaka kumtaja jina lake kwa sababu za kiusalama na kutoharibu upelelezi, kuwa msamaria mwema huyo alimwokota Dkt. Ulimboka katika msitu wa Mabwepande  uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na kutoa taarifa kituo cha Polisi cha Bunju, ambapo Askari  aliyekuwa zamu alichukua maelezo yake na baada ya hapo, alipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Kamanda Kova alisema Jeshi la Polisi Kanda Maalum limeunda jopo maalum kwa ajili ya uchunguzi na upelelezi wa tukio hilo la utekaji nyara, kwani ni tukio la kwanza kutoke nchini.

Ameongeza kwamba, wahusika wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo wachukuliwa hatua za kisheria na sheria itafuata mkondo wake ili kukomesha matukio mengine kama hayo.

                              Source: http://www.wavuti.com/#ixzz1z3XDAV7E

No comments:

Post a Comment