Pages

Saturday, December 29, 2012

SOME TEXT MISSING-01

Mara yangu ya kwanza kuishi Ilala, Dar es Salaam kwa muda mrefu ni pale nilipokwenda kumtembelea  kaka Luka wakati anaumwa miguu kiasi cha kushindwa kutembea hata hatua moja. 
Mbaya zaidi, katika kipindi hichohicho akapata ugonjwa wa kupooza ‘stroke’, hivyo wazazi wakaniambia nifunge biashara yangu ya genge,  pale Dodoma nije kumsadia shemeji.
Nilipokelewa na mke wa kaka, mama Lilian ambaye alinishukuru sana kwa uamuzi wangu wa kuja Dar kwa kaka kwani itamsaidia yeye kufanya mambo mengine ambayo yalilala kwa sababu ya mumewe kuugua miguu na kupooza.

Kaka alikuwa hawezi kwenda chooni, kwenda bafuni bila kupelekwa na mbaya zaidi kazini kwake, walishamtosa kiaina kwani misaada ilipungua tofauti na zamani.
“Vipi nyumbani lakini, hajambo baba, mama?” kaka aliniuliza.
“Kusema ukweli kaka wote wazima, ila baba naye alikuwa akisumbuliwa na macho, lakini kwa sasa yuko sawasawa.”
“Asante sana kwa taarifa, mimi kama unavyoniona, ni muda mrefu naumwa, niko ndani tu.”
“Pole sana kaka.”
“Asante mdogo wangu.”


Kwa ujumla maisha pale nyumbani kwa kaka yalionekana ni bomba. Kwani usafiri mzuri ulikuwepo, nyumba kubwa ya kisasa, wafanyakazi wawili, mmoja wa shughuli za ndani, mwingine wa kuweka sawa mazingira kwa ujumla.
Niligundua baada ya kaka kuumwa, gari alikuwa akiliendesha shemeji.
Jambo moja nilijiuliza moyoni, kama kaka anaumwa kwa muda mrefu ugonjwa wenyewe ni ule. Je, shemeji anajikidhi wapi mambo yake ya mapenzi? Maana naye ni binadamu.

***
Wiki moja baada ya kuanza maisha pale, shemeji alionekana kama kunibadilikia, alionesha dalili zote kwamba hanipendi na anaombea niondoke maana siku moja aliniuliza kwa macho makavu…
“Hivi shemeji utaondoka lini?”
“Ah! Shemeji, nitaondoka na hali ya kaka iko hivi..?”
“Kwani wewe daktari?”
“Hata kama siye, lakini siwezi kuondoka, kwani shemeji nakusumbua kuwepo hapa nyumbani?”
“Mimi sijasema hivyo.”
Nilishindwa kumwelewa shemeji, lakini pia sikumwambia kaka wala kuwajulisha wazazi kule Dodoma.
Siku moja usiku wa saa sita, alikuja chumbani kwangu akanigongea mlango, nikajua kaka amezidiwa, nikatoka nikiwa ndani ya bukta tu…

“Shemeji kuna kitana huku kwako?”
Kabla sijamjibu niliangalia kichwani kwake, alikuwa na nywele ndefu, tena amezitia dawa, sasa kitana cha nini…
“Sina shemeji, si unajua nywele zangu hizi, hazihitaji kitana,” nilisema huku nikijishika kichwani kwa kupapasa.

Aligeuza bila kuendelea na mazungumzo na mimi, nikarudi chumbani, lakini nilisahau kufunga mlango.
Nilijitupa kitandani nikawa najiuliza shemeji alitaka kitana cha nini…
“Au kaka kazidiwa sasa anataka kumpeleka hospitali ndiyo anataka kumchana nywele?”
“Lakini kama ni hivyo, kwanini asiniite na mimi katika msafara?”
Mara mlango ukagongwa tena…
“Ngo ngo ngo…”
 “Karibu,” niliitika kwa sauti ya chini maana bado nilikuwa niko kwenye mawazo ya ujio wa kwanza.
Safari hii, shemeji alisukuma mlango akaingia ndani. Uso wake ulionesha ujasiri na ukali, nikahisi amekuja kunifokea kuhusu jambo fulani…

“Hivi kuna kiberiti huku kwako shemeji?”
“Mh! Sijakiona shemeji.”
“Kule mbona hakipo?”
“Wapi, jikoni?”
“Jikoni, kote pia nimekitafuta sijakiona.”
“Dada wa kazi anasemaje?”
“Sijamuuliza, nikajua labda kiko kwako.”

“Huku sidhani shemeji,” nilimjibu huku nikiwa napangua baadhi ya vitu kukitafuta. Lakini hadi mwishi, kiberiti hakikuonekana.
Shemeji aliondoka bila kuaga nikajua amekasirika sana, nilifunga mlango kwa funguo, nikarudi kitandani nikiwaza…
“Kesho nimwambie kaka nataka kurudi nyumbani, ni kazi sana kuishi katika mazingira haya, mtu hampatani sasa tutaishi vipi…

“Nadhani ananitafutia kisa ili anifukuze, ndiyo maana anauliza mambo mengi, mara kitana, mara kiberiti.”
Sijui ni wakati gani nilipitiwa na usingizi, ila nilikuja kushtuka kwenye saa kumi alfajiri baada ya kuhisi kitasa cha mlango kinazungushwazungushwa…
“Nani tena saa hizi?” nilijiuliza nikiwa naangalia saa ya kwenye simu.

Nilikwenda kuufungua mlango, shemeji alisimama mlangoni akiwa ndani ya khanga moja tu, tena aliifunga kwa kukatiza kwenye matiti yake…
“Shikamoo shemeji…”
“Marhaba umeamkaje?”
“Sijambo.”
“Bado umelala?”

“Nilikuwa nimelala, nimeshtuliwa ulivyoshika kitasa.”
“Nilikuwa nataka kukutuma mahali.”
“Sawa shemeji, ngoja nitoke basi.”
Niliruidi chumbani, nikavaa suruali juu ya bukta maana wakati naamka nilikuwa na bukta tu.

Nilipomaliza kuvaa bukta nilitafuta fulana ambayo ingekuwa rahisi kuivaa mwilini na kutoka, nikaipata. Wakati natoka, ile nashika mlango tu, nikakumbana na shemeji naye akiingia, ina maana safari hii alikuwa akiingia bila hodi...
“Karibu shemeji.”

“Asante,” aliitikia kwa sauti ya chini sana...
“Umeshajiandaa?” aliniuliza...
“Ndiyo shemeji.”
“Safari yenyewe nimeiahirisha, pengine mpaka baadaye sana, nitakwambia.”
“Sawa shemeji.”
Nilimwona shemeji akitaka kugeuka ili atoke, lakini kabla hajafanya hivyo, akaniangalia kwa macho yaliyojaa maswali au wasiwasi...

“Unajua kaka yako anaumwa?” aliniambia.
“Amezidiwa?” nilimuuliza nikiamini hali ni mbaya ndiyo maana alikuwa akitafuta kitana usiku...
“Kuzidiwaje?”
“Si umeniambia kaka anaumwa sana?”
“Kwani we hujui kama anaumwa?”
“Najua, sasa si umesema anaumwa zaidi?”
“Mimi nimesema anaumwa zaidi au nimekuuliza unajua kama kaka yako anaumwa?”
“Najua shemeji.”
“Basi ukae ukijua kaka yako anaumwa, mimi ni binadamu kwa hiyo naomba nichukuliwe kwa ubinadamu wangu ulivyo.”
Sikumuelewa shemeji alikuwa na maana gani kusema vile. Kwani nijuavyo mimi nilikuja Dar kwake kwa ajili ya kumsaidia kumuuguza kaka Luka...
“Shemeji si ndiyo maana nipo Dar kwa ajili hiyo.”

“Mbona sioni mchango wako.”
“Ah! Shemeji lini nimekataa kukusaidia?”
“Siku zote tangu ulipokuja,” aliniambia, lakini kitu cha ajabu nilimwona akiachia tabasamu laini huku akiniangalia kwa macho yaliyojaa uchovu.

Nilishindwa kujizuia na mimi nikacheka huku nikimwangalia kwa woga. Lakini kitu kimoja nilihisi kuna kitu, mazungumzo yake hakuwa akitoa sauti ya juu. Ilikuwa kama vile hataki watu wajue yuko chumbani kwangu.

“Shemeji nakuja sasa hivi usitoke,” aliniambia akitoka kwa haraka.
Nilikaa kitandani, nikawaza...
“Mh! Hapa pana ishu, tena ishu yenyewe inaweza kuwa ya ajabu.”
Mara mlango ulisukumwa, akarudi tena akiwa tofauti na alivyokuwa mara ya kwanza...
Na IRENE MWAMFUPE NDAUKA.

No comments:

Post a Comment