Pages

Tuesday, January 29, 2013

Mwanafunzi agongwa na kufa Wilayani Bunda

JESHI la Polisi wilayani Bunda linamshikilia Elifinya Batholomeo (28), mkazi wa jiji la Dar es Salaam kwa tuhuma za kumgonga mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kabalimu, Maria Peter (7), na kusababisha kifo.

Tukio hilo limetokea juzi saa 10:00 jioni katika eneo la mtaa wa Posta, barabara ya Musoma –Mwanza, ambapo mwanafunzi huyo alikuwa akitembea kando ya barabara.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo gari hilo lilikuwa katika mwendo kasi wakati likipishana na gari jingine ndipo lilipomgonga mwanafunzi huyo ambaye alikufa papo hapo.
Walisema kuwa dereva huyo ambaye alikuwa akiendesha gari aina ya Pajero lenye na T 651 

BMZ mali ya kampuni ya Geodata, baada ya kubaini kuwa ameua, hakusimama kutokana na kuhofia maisha yake.
Aidha mashuhuda hao walilazimika kutoa taarifa polisi ambao walifika na kuchukuwa mwili wa mwanafunzi huyo ambao umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya.
Walisema kuwa baadaye polisi walilifuatilia gari hilo ambalo lilipitia njia za mkato na kufanikiwa kulikamata katika kijiji cha Nyamatoke.

Akizungumzia tukio hilo mama wa mwanafunzi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Ghati Wambaura alisema kuwa mtoto wake aliondoka siku hiyo asubuhi kwenda kanisani lakini majirani walimpa taarifa juu ya kugongwa na gari.
“Mtoto wangu huwa anashinda kanisani na wenzake lakini ilipofika jioni niliambiwa na watu kuwa kuna mtoto amegongwa na nilipoenda polisi na kujulishwa kuwa mwili upo hospitali ndipo nilipobaini kuwa ni mtoto wangu,” alisema.
Polisi walisema kuwa wanatarajia kumfikisha mahakamani dereva huyo ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

No comments:

Post a Comment