Pages

Tuesday, February 26, 2013

Mama Kanumba alia na kalenda za mwanaye

MAMA mzazi wa aliyekuwa msanii nyota wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba, Flora Mtagoa, amelalamikia kitendo cha mtu aliyetengeneza na kusambaza kalenda zenye picha ya mtoto wake bila idhini yake.

Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Flora alisema ni bora yule aliyetoa kitabu, alifanya ustaarabu pamoja na Zamaradi Mketema aliyetoa ‘CD’ iliyokwenda kwa jina la ‘Neno la Mwisho’ ambao walifuata taratibu na ridhaa, kisha kumlipa fedha aliyotaka.

“Zamaradi na yule aliyechapa kitabu cha Kanumba, hawa walikuja wakazungumza na mimi nikawatajia fedha niliyotaka wakanilipa bila ubishi, lakini huyu mtu aliyefyatua kalenda za mwaka huu, yeye hana ustaarabu, kwani amejifanyia kiholela tu kwa kutumia jina la mtoto wangu bila ridhaa yangu na hajailipa familia chochote, hii si sawa,” alilalamika Flora.

Aliviomba vyombo vya habari vimsaidie kumtafuta mhusika huyo kwa sababu hata namba walizoziandika chini ya kalenda hizo zikipigwa hazipatikani.
Aliongeza kuwa baada ya kifo cha mwanaye, wapo watu wengi waliofaidika huku wengine wakitangaza kuwa wamevunja rekodi ya mauzo lakini bila hata kwenda kuipa familia kiasi chochote cha fedha kama pole.

“Mwanangu, wapo wengi waliofaidika kibiashara na kifo cha Kanumba, pia wapo wengine ambao walidiriki kutangaza hadharani kwamba wamevuka malengo, inasikitisha sana,” alisema.Hivi sasa Flora anajipanga kuadhimisha mwaka mmoja tangu kijana wake Steven Kanumba alipofariki dunia Aprili 7, mwaka jana nyumbani kwake Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment