Pages

Tuesday, February 26, 2013

Waziri amuondoa, aagiza katiba mpya ifutwe, itumike ya zamani

SERIKALI imemuondoa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo nchini na kuagiza kufutwa kwa katiba mpya ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na badala yake itumike ile ya mwaka 2006.

Hatua hiyo, imekuja baada ya hivi karibuni kuibuka kwa utata juu ya katiba mpya ya TFF, iliyopitishwa kwa njia ya waraka, wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo uliopangwa kufanyika Februari 24 na ule wa Bodi ya Ligi Februari 22, kabla ya kusitishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alisema kuwa ameamua kumteua msajili mpya, baada ya aliyekuwepo kupitisha katiba mpya ya TFF kinyume na utaratibu.
Alisema kuna mengi yalijitokeza ikiwemo baadhi ya wagombea kulalamikia kuenguliwa, hivyo wizara iliamua kuliangalia hilo kwa uzito unaostahili na kuamua kuchukua hatua stahiki.
             Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara
Mukangara alisema sheria Na.12 ya BMT na marekebisho yake Na.6 ya mwaka 1971 pamoja na kanuni za BMT na kanuni za usajili Na. 442 mwaka 1999 zimekiukwa.

Alisema kuwa zipo taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) litakuja Tanzania, hivyo anamuelekeza Msajili na anailekeza TFF kuitaarifu kuhusu maelekezo hayo ya kutumia katiba ya mwaka 2006, na waambiwe hali halisi iliyojitokeza.
Mukangara alisema anaielekeza TFF iitishe mkutano mkuu kwa msingi wa katiba yao ya mwaka 2006 na kanuni za BMT na wafanye uchaguzi kwa mujibu wa katiba hiyo kwa kuzingatia sheria za BMT.

Alisema kanuni ya BMT Na.11(1), inaeleza wazi utaratibu wa marekebisho ya katiba haikufuatwa, kwani kimsingi, TFF ilitakiwa ijaze fomu Namba 6,7,8 na 9 kwa mujibu wa sheria na kanuni za BMT.
Mukangara alisema kimsingi upo utaratibu wa kurekebisha katiba za vyama vya michezo, kwa mujibu Sheria ya Baraza la Michezo iliyotungwa na Bunge, na kanuni zake ziko wazi na ni rahisi kuzielewa.

“Sasa TFF hawakufuata taratibu kwa mujibu wa sheria na kanuni za BMT.
“Baada ya kupitia taarifa mbalimbali za BMT, nimejiridhisha kuwa katiba itakayotumika ni ile ya mwaka 2006, ikiwa ni pamoja na TFF kuitisha mkutano mkuu na kutumia katiba ile ile ya mwaka 2006,” alisema Mukangara.
Alisema kwa mamlaka aliyonayo, anaagiza msajili awajulishe TFF, kufuta matumizi ya katiba ya mwaka 2012 na watumie ya mwaka 2006 na barua ilifikie shirikisho hilo kabla ya saa 7 mchana, jana.
Waziri huyo, alitoa maagizo kwa msajili kufuata taratibu za usajili kwa mujibu wa sheria na kanuni za BMT.

Alibainisha kuwa kuna taarifa ya uwezekano wa FIFA, ikachukua hatua kali juu ya serikali kuingilia, kitu ambacho amedai si kweli.
Mukangara aliongeza kuwa kila nchi ina Katiba yake, hivyo si kweli kama FIFA wanaweza kuifuta Katiba ya nchi.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, kuhusu uamuzi wa serikali, alisema ni mapema mno kwao kusema lolote hadi pale watakapopata rasmi taarifa hiyo.
“Hatuwezi kusema lolote, kwani hatujapata taarifa rasmi ya serikali tujue kama ni maoni, ushauri au agizo. Tukishajua ni kitu gani, TFF kama taasisi ndipo kwa kutumia vyombo vyake vya maamuzi, itatoa uamuzi na msimamo wake,” alisema Osiah.
Hata hivyo akaongeza kuwa kama ni agizo hakuna tafsiri nyingine ya kilichofanyika, isipokuwa serikali kuingilia masuala ya uendeshaji wa soka, jambo ambalo limekuwa likipingwa na FIFA.

No comments:

Post a Comment