Pages

Friday, March 29, 2013

Mzazi aeleza chanzo cha wanafunzi kufeli kidato cha nne mwaka jana.

MWENYEKITI wa Wazazi Wilaya ya Babati Vijijini, Willy Bayo, amesema matokeo mabaya kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana yametokana na mitaala mibovu ya kufundishia pamoja na kuzibwa kwa mianya ya uvujaji wa mitihani iliyokuwa ikifanywa na baadhi ya walimu nchini.

Bayo alitoa kauli hiyo juzi wakati akichangia mada kwenye kikao cha wadau wa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Manyara, kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Alisema pamoja na matokeo hayo kuwa ni janga la kitaifa inapaswa serikali ielewe kwamba tatizo hilo limechangiwa na kuzibwa na kudhibitiwa kwa uvujaji wa mitihani uliokuwa ukifanywa na baadhi ya walimu kwenda kwa watahiniwa nchini.
Alibainisha kwamba tegemeo la kuvuja kwa mitihani kuliwafanya pia walimu kutokuwa na ari ya kufanya kazi kwa kutegemea kuwa mwisho wa masomo mwanafunzi atafaulu kwa kununua mitihani.

“Mfano hai kwa wilaya hii tulikuwa tukiwaona wazazi wa wanafunzi waliokuwa wakitaka kufanya mitihani wakipanga foleni kwenye migahawa na kila mmoja alikuwa akitozwa kuanzia sh 20,000, wakisubiri walimu ili wapatiwe mitihani kwa ajili ya watoto wao.
“Utakuta mwanafunzi amefaulu darasa la saba kwenda kidato cha kwanza lakini hajui kusoma wala kuandika, unajiuliza alifanya vipi mtihani mpaka akafaulu, kumbe alipata fursa ya kufanyiwa mtihani na kupewa majibu,” alifafanua Bayo.

No comments:

Post a Comment