Pages

Friday, March 29, 2013

Mtoto Debora Riziki (3) auawa, azikwa sebuleni katika nyumba yao.

MTOTO Debora Riziki (3), mkazi wa Kijiji cha Isange wilayani Rungwe, ameuawa na mwili wake kuzikwa sebuleni katika nyumba yao.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya 7:40 mchana na anayetuhumiwa kuhusika na mauaji hayo ni baba mzazi wa mtoto huyo, Riziki Mwangoka (27).

Alisema sababu ya kufanya ukatili huo ni kutokana na mgogoro wa kindoa kati ya baba huyo na mama wa mtoto huyo, Esther Msafiri Mwambenja (23), mkazi wa Kijiji cha Kimbukwe.
Kamanda Diwani alisema kutokana na mgogoro wa muda mrefu wanandoa hao walitengana na kwamba siku ya tukio baba huyo alifika nyumbani kwa mzazi mwenzake na kumchukua mtoto huyo kwa nguvu na kwenda kumuua.

Alisema mwili wa marehemu umeshafanyiwa uchunguzi na umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi. Polisi wanaendeea na utaratibu kwa ajili ya kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.
Kamanda Diwani alitoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi ili kuepusha matatizo yanayoweza kuepukika.

No comments:

Post a Comment