Pages

Tuesday, March 26, 2013

Wema amnusuru Kajala jela

MSANII mahiri wa filamu hapa nchini, Wema Sepetu, amemnusuru mwenzake Kajala Masanja, kwenda jela baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumhukumu kifungo cha miaka minane au faini ya sh milioni 13.

                                                                 Kajala Masanja
Kajala alitiwa hatiani katika makosa ya kula njama kuhamisha umiliki wa nyumba iliyokuwa imezuiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali isiuzwe.

Hukumu hiyo, ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, ambapo alianza kwa kuikumbusha mahakama hiyo kuwa Kajala na Faraja Chambo, walikuwa wakikabiliwa na makosa matatu yaliyofunguliwa mapema mwaka jana mahakamani hapo.

Makosa hayo ni kula njama kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, ambapo washtakiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo la kula njama la kuhamisha umiliki wa nyumba iliyoko Kunduchi, Salasala, eneo ambalo halijapimwa jijini Dar es Salaam.

Shtaka la pili ni kwamba Aprili 14 mwaka 2010 walihamisha isivyo halali, umiliki wa nyumba hiyo, ambayo walikuwa wakiimiliki kwenda kwa Emilian Rugalia, ambaye ndiye walimuuzia kinyume na kifungu cha 34(2)A(3), cha Sheria ya TAKUKURU ya mwaka 2007 na shtaka la tatu ni la kutakatisha fedha ambalo walilitenda siku hiyo ya Aprili 14, 2010, huku wakijiua ni kinyume cha sheria.

Hakimu Fimbo alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, upande wa jamhuri umeweza kuithibitisha kesi hiyo na hivyo mahakama hiyo imemtia hatiani Kajala katika kosa la kwanza na la pili tu, wakati Chambo amepatikana na hatia katika makosa yote matatu.

Alisema, katika kosa la kwanza, Kajala na Chambo watatakiwa walipe faini ya sh milioni tano kila mmoja au kwenda jela miaka mitatu. Kosa la pili watatakiwa walipe faini ya sh milioni nane au kwenda jela miaka mitano kila mmoja.
Aidha katika kosa la tatu ambalo Chambo amekutwa na hatia peke yake, atatakiwa alipe faini ya sh milioni 200 au kwenda jela miaka mitano na kwamba adhabu hizo hazitakwenda pamoja. Hivyo Kajala peke yake amehukumiwa kwenda jela miaka nane au kulipa jumla ya sh milioni 13.

“Mahakama imewakuta na hatia washtakiwa wote katika kosa la pili kwa sababu ushahidi umethibitisha kuwa washtakiwa wote walikuwa wakifahamu kuwa kulikuwa na hati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliyokuwa imezuia nyumba yao wasiiuze kwa sababu Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa ilikuwa ikidai kuwa nyumba hiyo imepatikana kwa njia ya utakatishaji fedha, lakini wao wakakaidi amri hiyo wakaamua kuiuza,” alisema Hakimu Fimbo.

Akilichambua kosa la kwanza, alisema pia upande wa jamhuri umeweza kulithibitisha kwa sababu kosa la pili limeweza kuthibitishwa.
Kuhusu shtaka la tatu, hakimu huyo alisema amemwachilia huru Kajala kwa sababu upande wa jamhuri umeshindwa kuthitisha alishiriki vipi katika upatikanaji wa fedha haramu, kwa sababu ilidaiwa kuwa Chambo alizipata fedha haramu katika maelezo ya onyo kuwa alizipata fedha za kujengea nyumba hiyo wakati akiwa mfanyakazi wa NBC.
“Na kwa mujibu wa maelezo ya onyo la Chambo, ambaye ni mume wa Kajala, alikiri kuwa wakati akiwa mfanyakazi wa NBC, alikuwa akichukua fedha na kuzituma kwa baadhi ya watu wa ofisi ya TTCL, watu ambao hawakuwa wakistahili kulipwa na baada ya vyombo vya dola kuanza kumfuatilia, akaamua kuiuza nyumba yake hiyo,” alisema Hakimu Fimbo.
Baada ya hukumu kutolewa, wasanii wa filamu nchini walikuwa wamefika mahakamani hapo kufuatilia hukumu hiyo, walikusanyika katika viunga vya mahakama hiyo na kuanza kujadiliana ili wachangishana fedha.
Lakini Wema, aliwataka wenzake wasichangishane, badala yake yeye analipa sh milioni 13 na kuondoka katika eneo hilo na kisha kurejea mahakamani hapo majira ya saa saba mchana na kulipa faini hiyo, kisha kuondoka na Kajala, wakati Chambo akirudishwa gerezani kwa kushindwa kulipa faini hiyo, pia anakabiliwa na kesi nyingine ya utakatishaji fedha mahakamani hapo.

No comments:

Post a Comment