Pages

Friday, May 31, 2013

Madaktari wa mifupa warejea nchini

MADAKTARI Bingwa wanne kati ya 20 waliopelekwa nje ya nchi kwa nyakati tofauti kujifunza zaidi kuhusu upasuaji na utaalam wa mifupa wamerejea.

Kurejea kwa madaktari hao kulibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif Rashid wakati akifungua mafunzo ya upasuaji kwa madaktari bingwa 80 kutoka nchi mbalimbali Afrika.

Mafunzo hayo yanafanyika kwenye Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) chini ya udhamini wa taasisi za Sign Fructure Care International, Chuo Kikuu cha Saint Francisco, 
AO Foundation zote za Marekani wakishirikiana na uongozi wa MOI.
“Serikali inalielewa tatizo la ukosefu wa wataalamu bingwa wa upasuaji na mifupa ndiyo maana tuliwapeleka 20 nje ya nchi kujiendeleza sasa wanne kati yao wamesharudi.

“…Lakini mchakato wa kuwaandaa wataalamu hawa ni mrefu kidogo, kwa sababu lazima wamalize masomo yao ya kawaida ya udaktari kabla ya kuwa wataalamu mabingwa,” alisema.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo alielezea juhudi za serikali kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoikabili MOI na hospitali nyingine ikiwemo msongamano wa wagonjwa kutokana na ongezeko la ajali nchini.

Alisema sababu ya serikali kujenga jengo la kisasa jirani na MOI linalotarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu, litapunguza msongamano wa wagonjwa wodini kwa vile litakuwa na uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Profesa Lawrence Museru, alisema mafunzo hayo yatawasaidia madaktari wake kwa maelezo kwamba kila kukicha fani ya upasuaji inaibuka na mambo mapya.

No comments:

Post a Comment