Pages

Tuesday, May 14, 2013

‘Serikali Afrika zisaidie wakulima wanawake’

SERIKALI barani Afrika zimetakiwa kutoa msaada kwa wakulima wanawake kama bara hilo linataka kufikia maendeleo endelevu kijamii na kiuchumi.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vijijini wa Nigeria, Dk. Akinwumi Adesina, katika kongamano la kikanda la kilimo la Muungano wa Umoja wa Vyama vya Kilimo Kusini mwa Afrika (SACAU) na kuongeza kuwa ni muhimu serikali na wadau wengine wanaosaidia maendeleo ya kilimo wakajua kuwa wakulima wengi katika bara hilo ni wanawake.

Kongamano hilo litakaloangalia kwa undani suala la jinsi ya kuhudumia kifedha kilimo cha Afrika linatayarishwa na Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT) kwa kushirikiana na SACAU.

“Wakulima wanawake wanahitaji kupata mikopo nafuu, uhakika wa ardhi, na teknolojia,” alisema na kuongeza kuwa mustakabali wa sekta ya kilimo katika bara la Afrika sio wa uhakika kama wanawake wakulima watawekwa pembezoni na mipango ya maendeleo inayohusu sekta hiyo.

Kongamano hilo linaloangalia kwa undani swala la jinsi ya kuhudumia kifedha kilimo cha 
Afrika linatayarishwa na Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT) kwa kushirikiana na SACAU.
Waziri huyo alisema hakuna sababu ya bara la Afrika kuagiza chakula toka nje wakati zaidi ya asilimia 60 ya ardhi inayofaa kwa kilimo na ambayo bado haijatumika iko katika bara hilo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa SACAU, Ishmael Sunga, alisema wakulima wa Afrika hawawezi kuendelea kwa haraka na kuwa wakubwa kama hawataweza kupata huduma za uhakika za kifedha.

Mkurugenzi wa maendeleo ya mazao toka Wizara ya Kilimo, Usalama wa Chakula na Ushirika, Dk. Mshindo Msolla, alisema ni muhimu kwa serikali za Afrika zikajitahidi kuwa na usalama wa chakula katika kila nchi kabla ya kufanya lolote.
Akizungumza kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo, Dk. Msolla alisema serikali ya Tanzania inafanya juhudi kubwa kufikia mapinduzi ya kilimo kupitia mipango mbalimbali kama Kilimo Kwanza na mpango maalumu wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT).

No comments:

Post a Comment