Pages

Tuesday, May 14, 2013

Vijiji 91 Bukoba havina maji - Mbunge JIBU LA SWALI LA MBUNGE Bukoba vijijini.

VIJIJI 91 katika jimbo la Bukoba Vijijini vinakabiliwa na ukosefu wa majisafi na salama jambo ambalo linasababisha uzalishaji kushuka.

Hayo yalielezwa bungeni jana na mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza (CCM), alipouliza swali la nyongeza kwa kutaka serikali ieleze ni lini itapeleka maji katika vijiji hivyo.

“Jimbo la Bukoba Vijijini lina vijiji 92; ni kijiji kimoja tu ambacho kina maji, nataka kuelezwa ni lini wananchi wa vijiji 91 wataweza kupatiwa maji ambao waliamua kujitolea kuchanga fedha kwa ajili ya kununua mashine ya kuchimba visima?” alihoji Rweikiza.

Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kuelewa ni kwa nini vijiji vya Kibona Ibwera, Rukindo Kitahya na Katale havikupewa kipaumbele katika kutekeleza mradi wa maji kutokana na ukubwa wa tatizo hilo katika wilaya ya Bukoba Vijijini.
Aidha, alitaka kuelezwa ni lini serikali itatekeleza miradi hiyo, ili kuwaondolea kero ya kukosa majisafi na salama.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Kassim Majaliwa, alisema halmashauri ya wilaya ya Bukoba Vijiji imekamilisha usanifu wa miradi katika vijiji 10 walivyochagua kama vipaumbele vyao.
Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Kibirizi, Itongo, Lukindo, Katale, Mashule, Kitahya, Ibwera na Kyamulaile.

“Ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mashule umekamilika Machi mwaka huu na wananchi wanapata huduma ya maji, halmashauri inakamilisha taratibu za kusaini mkataba wa mkandarasi wa ujenzi wa mradi katika kijiji cha Kyamulaile na taratibu za manunuzi kwa ajili ya kuwapata makandarasi wa ujenzi kwa ajili ya vijiji viwili vya Kibana na Kitahya zinaendelea,” alisema.
Aidha alisema ujenzi wa mradi wa Bituntu, Kibirizi, Itongo, Lukindo, Katale na Ibwera utafanyika katika mwaka wa fedha wa 2013/14 ambapo sh bilioni 1.3 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema katika mwaka 2001/13, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ilitengewa sh milioni 612.02 na hadi sasa sh milioni 416 zimeshatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.

No comments:

Post a Comment