Pages

Saturday, May 4, 2013

Serikali yakanusha Tanzania kuongoza kwa rushwa.

SERIKALI imekanusha taarifa zinazoeleza kuwa Tanzania inaongoza kwa vitendo vya rushwa na urasimu barabarani.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu, Mkiwa Kimwanga (CUF).

Katika swali hilo, mbunge huyo alitaka kujua ni lini serikali itaondoa vitendo vya urasimu na rushwa vilivyokithiti nchini na kuifanya Tanzania kuongoza.

Akiendelea kujibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema si kweli kwamba Tanzania inaongoza kwa vitendo hivyo, kwani rushwa ni tabia ya mtu.

Katika swali la msingi, mbunge huyo alihoji hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuondoa adha ya urasimu unaolalamikiwa na wadau wa usafirishaji na wafanyabiashara nchi jirani wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam.

“Kwa muda mrefu sasa wadau wa usafirishaji na wafanyabiashara wa nchi jirani wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam wamekuwa wakilalamikia urasimu uliopo barabarani unatokana na vituo vingi vya mizani, TRA na kusimamishwa mara kadhaa na askari wa usalama barabarani, jambo linalowafanya kuchelewa bandarini na ama kuharibika kwa bidhaa walizobeba,” alisema mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri alisema kulingana na sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 2001 magari yote yenye uzito kuanzia tani 3.5 na kuendelea yanatakiwa kuingia kwenye vituo vya mizani na kupima uzito wakati wa safari zao.
Alisema lengo kuu la kupima magari ni kulinda barabara na madaraja ambayo ujenzi wake unagharimu taifa fedha nyingi sana.

Aidha alisema Tanzania kuna vituo saba vya mizani kwenda Kisumo na si 30 kama alivyosema mbunge na kuongeza kuwa hivyo vingine havijui.

“Katika kuboresha shughuli zinazofanywa katika vituo hivyo vya mizani, serikali imejipanga kununua mizani ya kisasa, ili kuboresha utendaji kazi na kuifanya kazi hiyo kuwa rahisi,” alisema Lwenge.

No comments:

Post a Comment