Pages

Saturday, May 4, 2013

Wasiosikia walalamika kukosa habari kwenye runinga.

WALEMAVU wasiosikia wamelalamikia kutopata haki ya habari katika vituo vya televisheni kutokana na kukosekana kwa wataalamu wa lugha za alama.

Walemavu hao walitoa kilio hicho jijini Dar es Salaam jana wakati Klabu ya Waandishi Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) walipotembelea makundi ya maalumu yale ya walemavu na watoto waishio katika mazingira maalumu katika kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Walisema vitu ambavyo vinatokea huko wao hawajui kutokana na kutokuwapo na wataalamu wa lugha ya alama ambao ndio wangekuwa kuwafikishia taarifa kwa njia hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea Shule ya Viziwi Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Kuwahudumia Viziwi Tanzania na Kaimu Mkurugenzi wa Shule ya Msingi Buguruni-Viziwi- Yassini Mawe, alisema suala la habari linaonekana halipewi kipaumbele kwa kundi hilo.

Alisema kuwa wamepata elimu ya kutosha katika uchaguzi wa Kenya kwa kuwa kulikuwapo na wataalamu wa lugha ya alama kwenye vituo vya televisheni.

Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa Dar es Salaam (DCPC), Benjamin Masese, alisema maadhimisho hayo yawe chachu kwa jamii katika kutoa habari zao, ili ziweze kufikika katika mamlaka husika.

Wakati huohuo, Kambi ya Wazee ya Nunge, Kigamboni ilikataa msaada pamoja na kuzungumza na waandishi wa habari kwa madai kuwa viongozi wa klabu ya waandishi hawakutoa taarifa ya ujio wao, hivi kulazimika kupeleka msaada huo kwa watoto waishio katika mazingira magumu katika kituo cha Songambele Pamoja.

Wakati huohuo, waandishi wa habari nchini, wamesema uhuru wa vyombo vya habari nchini hauwezi kupatikana bila kuwepo utaratibu maalumu unaowafanya waweze kunufaika na taaluma yao.
Mwandishi wa Redio Uhuru, Cosmas Hinju, alisema waandishi wa habari wamekuwa kama ‘punda’ kutokana na kutolipwa stahiki zao kwa wakati muafaka, hali inayowafanya kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo rushwa.

Mhariri wa mtandao wa habari mpya.com, Odoyo Jackson, alisema uhuru wa vyombo vya habari nchini uko mashakani kwa kuwa baadhi ya wanahabari wameingia kwenye vikundi vya siasa.
Mwandishi wa gazeti la Mtanzania, Arodia Peter, alisema anaiona siku hiyo kama kiza kinene kwa kuwa waandishi wa habari hawana uhakika na maisha yao, kwani kuna makundi ya watu wameziweka roho za wanahabari rehani.
 

No comments:

Post a Comment