Pages

Wednesday, May 1, 2013

Walimu wapya wakesha kwa mkurugenzi.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, walimu wapya wa shule za sekondari wilayani Magu, mkoani Mwanza, juzi walilazimika kulala nje ya Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Magu, wakishinikiza kulipwa mishahara yao.

Walimu hao wapatao 100 kutoka shule mbalimbali wilayani hapa, walifikia uamuzi huo baada ya kutolipwa mishahara yao na haki zao nyingine stahiki tangu Machi mwaka huu, walipoajiriwa na serikali.

Wakizungumza nje ya ofisi hiyo, walimu hao walieleza kuchukizwa na kitendo cha serikali kutowalipa mishahara kwa muda wote huo.
Walisema kuwa kati ya walimu wapya 154, ni walimu zaidi ya 50 pekee ndio wameingizwa kwenye mpango wa kulipwa mishahara, huku wengine wakiwa hawajui hatima yao.
Walifafanua kuwa ofisi ya mkurugenzi imekuwa ikikataa kuzungumza nao na wakati mwingine inawaamuru waende kuomba fedha za kujikimu kwa wakuu wao wa shule, jambo ambalo wakuu hao wanakataa.
 “Juzi tumekuja hapa kwa mkurugenzi saa 2:00 asubuhi kudai fedha zetu za mishahara. Lakini tulizungushwa na ofisa elimu takwimu wa wilaya, ambaye alitupa vitisho kwamba tunahatarisha ajira zetu iwapo tutaendelea kukaa hapa.

“Licha ya kwamba mkurugenzi jana hatukumkuta na kupewa vitisho hivyo, tulilazimika kuweka kambi na kulala hapa. Na leo hatutaondoka hapa mpaka kieleweke,” alisema Deusdedith Millanzi kwa niaba ya wenzake.
Walimu hao waliongeza kuwa kutokana na kukosa mishahara yao tangu waajiriwe Machi mosi mwaka huu, kwa sababu majina yao hayajaingizwa kwenye utaratibu wa malipo, wataendelea kuweka kambi na kulala nje ya ofisi hizo.

Walisema kuwa wamejionea mkanganyiko dhidi ya majina yao, ambapo baadhi ya majina yaliyopo Ofisi ya Utumishi Wilaya ya Magu yanaonesha hayamo kwenye mpango wa kulipwa.
Lakini kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya majina hayo yanaonesha yamo katika mpango huo wa kupata mshahara kama watumishi wengine wa serikali.

“Tumechoka kuzunguka. Hivi tumeletwa Magu kuja kuteseka? Na kwa mtindo huu wanatuweka kwenye mazingira magumu sana walimu wengi. Tutaishije hawatulipi?” alihoji mwalimu mwingine ambaye alikataa kutajwa jina lake.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Magu (CWT), Boniphace Maghembe, aliiambia Tanzania Daima kuwa madai ya walimu hao yapo sahihi na kuitaka serikali iwalipe mishahara na stahiki zao si vinginevyo.

Akizungumzia malalamiko hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ya Magu, Bonaventra Kiswaga, alikiri walimu hao kulala nje ya ofisi ya mkurugenzi wakishinikiza kulipwa mishahara yao.
Kiswaga alisema kulingana na unyeti wa madai ya walimu hao, ofisi ya mkurugenzi na Utumishi ya wilaya hiyo zinayafanyia kazi malalamiko ya walimu hao, hivyo kuwataka wavute subira wakati ufumbuzi wa tatizo hilo ukitafutwa.

No comments:

Post a Comment