Pages

Friday, May 31, 2013

Yanga yaongezewa mamilioni na Kilimanjaro Premium Lager, imewazadia sh milioni 25.

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Premium Lager, imewazadia sh milioni 25 mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, kwa kutwaa taji hilo.
Mbali na zawadi hiyo ya TBL, Yanga ilijihakikishia kitita cha sh milioni 70 kutoka kwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo, kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom, kwa kuibuka mabingwa.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi hiyo, Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema kwamba zawadi hiyo ni sehemu ya ahadi ya udhamini wao kwa timu itakayoshinda au kushika nafasi za juu.

“Kama wadhamini wa klabu kongwe za Yanga na Simba, tuliahidi kutoa sh milioni 25 kwa timu itakayotwaa ubingwa wa Ligi Kuu na sh milioni 15 kwa timu itakayoshika nafasi ya pili, hivyo kutokana na Yanga kutwaa ubingwa ndio tunaikabidhi fedha hizi,” alisema.
Kavishe aliongeza kuwa zawadi hiyo ni sehemu ya sh bilioni 1.5 za udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager kwa Yanga na imetolewa kwa lengo la kuhamasisha klabu kujitahidi kwa kushinda zaidi na kusaidia katika maandalizi yake kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.

“Na tulifanya hivi makusudi ili kuleta ushindani kwa timu hizi za Simba na Yanga, ili ziweze kufanya vema kwenye ligi hiyo ambayo imekuwa na ushindani mkubwa.
Yanga imekuwa ikicheza mpira mzuri kipindi chote cha msimu wa Ligi Kuu na hivyo kuibuka washindi.

Napenda kuwapongeza wachezaji, kocha na uongozi mzima wa Yanga kwa matokeo mazuri ya kushinda Ligi Kuu kwa mara ya 24 sasa,” alisema Kavishe.
Akipokea hundi hiyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, mbali ya kushukuru, 

alisema timu yao ni nzuri na yenye nguvu kutokana na uongozi imara, pamoja na udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager.
“Mafanikio yetu ya uwanjani ni kielelezo cha mafanikio pia ya bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa ujumla, ambayo imekuwa ikitusaidia sana. Bia hii imetoa mchango mkubwa sana katika kuipa timu msukumo uliopelekea mafanikio haya,” alisema.
Kwa ubingwa huo, Yanga itaiwakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, pamoja na michuano ya Kombe la Kagame, ambalo ni mabingwa watetezi.

No comments:

Post a Comment