Pages

Saturday, June 29, 2013

Hospitali ya Bugando kutibu saratani

SERIKALI imesema Hospitali ya Rufaa Bugando itaanza kutoa tiba ya saratani kwa mionzi hivi karibuni.
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Abdulla Juma Saadalla wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kassim Ahmed (CUF).
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua mpango wa serikali wa kuanzisha kitengo cha wagonjwa wa saratani katika mikoa mingine.

Dk. Saadalla alisema mashine hizo za kutibu kansa kwa mionzi zinatarajiwa kuwasili katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Agosti mwaka huu.
Alisema baada ya mashine hizo kuwasili, wagonjwa wenye matatizo ya saratani kutoka Kanda ya Ziwa wanaohitaji mionzi hawatalazimika kwenda Dar es Salaam kupata huduma hiyo.


Alisema kwa kutambua umuhimu wa kupeleka huduma hizo karibu na wananchi, serikali kwa kushirikiana na hospitali hiyo imeanzisha huduma za ngazi ya kitaifa katika hospitali hiyo ya Bugando.
“Awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo na uagizaji wa vifaa na mashine tiba kwa ajili ya huduma hizo imekamilika, mpaka sasa wagonjwa 4,000 wameshatibiwa,” alisema.

Alisema serikali itaendelea na juhudi za kusogeza huduma za afya za rufaa karibu na wanapoishi wananchi katika kanda nyingine na ngazi zote kadiri hali ya uchumi na mapato yatakavyoruhusu.
Alisema kwa sasa huduma kwa wagonjwa wa kansa zinatolewa kila hospitali za mikoa ingawa kwa viwango tofauti, na kwamba wagonjwa ambao hawawezi kutibiwa katika hospitali hizo hupewa rufaa katika hospitali za ngazi za juu ikiwemo Taasisi ya Kansa ya Ocean Road.

No comments:

Post a Comment