Pages

Saturday, June 29, 2013

Makaburi 250 kuhamishwa Dar


HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam imetangaza kuyahamisha makaburi 250 yaliyopo ndani ya eneo la mradi wa upanuzi wa njia za umeme Kata ya Manzese na Kata ya Ubungo, Mtaa wa Ubungo Kisiwani.

Hatua hiyo ilitangazwa jana na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mhandisi Mussa Natty katika taarifa yake kwa vyombo vya habari baada ya kupata taarifa ya kuhamisha makaburi hayo kutoka Shirika la Umeme Nchini(TANESCO).

Kutokana na hatua hiyo, amewataka watu wote wenye ndugu au jamaa waliozikwa kwenye eneo hilo kwenda kwenye ofisi za Ofisa Mtendaji wa Kata ya Manzese na Ubungo kujiandikisha wakiwa na barua ya utambulisho kutoka ofisi ya mtaa wanakoishi kabla ya Julai 25.

“Mkurugenzi wa TANESCO anawatangazia ndugu na jamaa za marehemu waliozikwa kwenye makaburi yaliyopo ndani ya eneo la mradi wa upanuzi wa njia za umeme Kata ya Manzese, Mtaa wa Madizini na Kata ya Ubungo Mtaa wa Ubungo Kisiwani, kwamba anakusudia kuhamisha makaburi 250 ili shughuli ya upanuzi wa njia ya umeme iweze kuanza,” alisema Natty katika taarifa yake.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya mitaa (Mamlaka za Miji) ya mwaka 1982, kanuni ya mwaka 2008 namba 46(c) Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni itasimamia zoezi hilo kwa kutumia wataalamu wake.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, makaburi hayo yatahamishiwa katika makaburi ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni yaliyopo Tegeta Kata ya Kunduchi baada ya tararibu zote kukamilika.

No comments:

Post a Comment