Pages

Saturday, June 29, 2013

Kashfa nzito Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam


HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam imeingia katika kashfa nzito baada ya kuvunja nyumba ya mwanamke mmoja Ashura Swed mkazi wa Upanga kwa maelezo kuwa ipo barabarani.

Katika hali ya kushangaza, manispaa hiyo imemruhusu kujenga eneo hilo hilo mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la Bahadur Dewji mwenye asili ya Asia.

Akizungumza na Tanzania Daima, mjukuu wa Ashura, Shamsa Salim ameiomba serikali kuingilia kati sakata hilo ili kuzuia kile alichodai kuwa uonevu wanaofanyiwa na watu wenye uwezo wa pesa.

Akisimulia huku akibubujikwa na machozi, Shamsa alisema Alhamisi ya wiki iliyopita walishangaa kuona nyumba yao namba 897 iliyoko Mtaa wa Mfaume, Upanga ikivunjwa huku wao wakiwa hawana taaarifa yoyote juu ya ubomoaji huo kwa madai kuwa ipo barabarani.

“Ilikuwa Alhamisi, wiki jana, majira ya saa tano asubuhi tulishtuka na kushangaa kuona kundi la watu waliojitambulisha kuwa wafanyakazi wa Manispaa ya Ilala wakivunja nyumba yetu. Tulipowaomba watupatie amri ya mahakama inayowaruhusu kuvunja nyumba yetu hawakutuonyesha badala yake waliendelea kuvunja tu.


“Kama wanadai kuwa nyumba yetu ipo barabarani, mbona jengo la SIDO halijabomolewa? Kama sio uonevu huu, ni nini jamani?” alisema kwa uchungu Shamsa.

Alisema kuwa bibi yake ambaye ni ajuza mjane, ni mmiliki halali wa nyumba hiyo hata kabla ya mumewe kufariki dunia Juni, 2009 na kuongeza kuwa kuvunjwa kwa madai kuwa wamevamia barabara na eneo lao kupewa mtu mwingine ni uonevu wa dhahiri kwa Mtanzania mnyonge.
Alisema wamefuatilia kwa siku kadhaa tangu wiki iliyopita walipoona ujenzi wa haraka unaanza na kubaini kuwa kuwa unafanywa na Dewji ambaye alidai anawanyima amani kwani amefikia hata kupiga risasi ili kuwatisha wasidai haki yao.

“Tulipoona tunanyang’anywa haki yetu tulienda kuchukua RB, tunayo na sasa tumefungua kesi, na kama huyo Dewji hilo ni eneo lake kwanini anafanya mambo ya ajabu ya kutunyima amani? Nina imani haki ya mtu haipotei, kwa kuwa sisi ni wamiliki halali wa eneo hili, na watu wasitumie fedha zao kutunyanyasa sisi wanyonge jamani,” alibainisha Shamsa.

Alisema kuwa walipoona hali si shwari usiku wa kuamkia Jumatatu, wiki hii walimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi ili awape msaada baada ya Dewji kufyatua risasi nne kuelekea katika nyumba yao.
Shamsa alisema kuwa Kamanda Minangi alifika kwa wakati katika eneo hilo akiwa na askari wake, lakini walishangaa kuona wakishindwa kumkamata mtuhumiwa wao na badala yake askari mmoja alianza kuwasihi walitupe ganda la risasi walilookota kwa maelezo kuwa wanaweza kugeuziwa kibao wakapata matatizo makubwa.
Amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Profesa Anna Tibaijuka kuingilia kati ili haki ipatikane.
Tanzania Daima lilimtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Mwendahasara Maganga ili kutolea ufafanuzi tuhuma hizo ambapo alisema kuwa hakuwa na taarifa yoyote kuhusu suala hilo na kumtaka mwandishi ampe muda ili alifuatilie kwa wasaidizi wake.
“Kwa kweli sina taarifa kabisa na suala unalonieleza, nipe muda niwasiliane na wasaidizi wangu, lakini ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba sisi ni taasisi inayofanya kazi kwa utaratibu, hatuwezi kumpa mtu au taasisi yoyote kibali cha kujenga eneo ambalo ni barabara. Huyo jamaa aliwaonyesha kibali cha kuruhusiwa kujenga? Kama hakuwaonyesha basi huyo ni mhuni tu, nipe nafasi nilifanyie kazi,” alifafanua Maganga.
Kwa upande wake Dewji anayedai kuwa mfanyakazi wa Aghakan Foundation, amedai kuwa eneo hilo wamepewa kihalali na manispaa ili wajenge barabara ya kutokea wanafunzi wa Sekondari ya Aghakan.
Naye Kamanda Minangi alikiri kupigiwa simu na Shamsa kupewa taarifa za Dewji kurusha risasi, lakini akadai kuwa taarifa hizo zilikuwa za uongo.
Lakini katika hali ya kushangaza Tanzania Daima lilipofika eneo la tukio liliona askari polisi wakiwa wamewekwa hapo kupiga doria, hali iliyothibitisha madai ya Shamsa kuwa kulikuwa na tatizo kubwa eneo hilo tofauti na maelezo ya kamanda Minangi.

No comments:

Post a Comment