Pages

Tuesday, August 20, 2013

‘Madereva wanaoharibu barabara wakamatwe’

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, amewaagiza viongozi wa Wilaya ya Kinondoni kuwakamata madereva wa magari na pikipiki wanaoharibu barabara inayojengwa kwa kupitisha vyombo vyao kwenye maeneo yasiyohusika.

Akizungumza Sadik, alisema serikali haitavumilia kuona barabara hiyo ikiharibiwa wakati fedha nyingi zimetumika.

Alisema viongozi hao ni lazima wasimamie sheria ipasavyo katika kuwadhibiti watu hao ambao vitendo vyao wanavyofanya ni sawa na wahalifu wengine.

Sadik alisema kila anayepitisha gari na pikipiki na wale wanaotumia maeneo hayo kwa kuwasha moto wajue wanavunja sheria, hivyo ni lazima wakamatwe mara moja.

“Watanzania ni lazima wajifunze ustaarabu wa kuthamini maendeleo yao, pia wajue fedha zinazotumika katika ujenzi wa barabara hii na nyingine zinatokana na kodi zao, hivyo waone uchungu kwa kuzitunza,” alisema Sadiki.

Alitoa wito kwa viongozi wa maeneo mbalimbali ambako serikali imeamua kuzijenga barabara zake kuhakikisha inawabaini wahalifu hao ambao wakiachiwa wanaweza kulirudisha nyuma kimaendeleo taifa hili.

No comments:

Post a Comment