Pages

Tuesday, August 20, 2013

Majambazi yavamia kituo cha mafuta.

Habari na na Julieth Mkireri, Pwani - Tanzania Daima.
WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamevamia na kupora fedha katika kituo cha mafuta cha Derina, kilichopo maeneo ya Picha ya Ndege, wilayani Kibaha, mkoani Pwani, kinachomilikiwa na mfanyabiashara David Mosha.

Majambazi hao wanaokadiriwa kufikia kumi, walikivamia kituo hicho baada ya kuwateka walinzi wa kituo hicho na kupora mali mbalimbali ambazo hadi sasa thamani yake haijajulikana.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani,  Urlich Matei, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema lilitokea usiku wa kuamkia Agosti 20, majira ya saa saba usiku.
Kamanda Matei alisema majambazi hao ambao walikuwa na silaha za moto, walikwenda katika kituo hicho cha mafuta wakiwa na  magari mawili, moja aina ya Prado na jingine aina ya Saloon, lenye rangi nyeupe.

Aidha, alifafanua kuwa majambazi hayo yalipofika yaliegesha magari hayo karibu kabisa  na pampu za kuwekea mafuta na baada ya hapo waliteremka na kuwaweka chini ya ulinzi walinzi waliokuwa zamu siku hiyo.

“Kitu ambacho walikifanya majambazi hao, walijifanya kama vile wanataka kuweka mafuta kumbe nia yao ilikuwa kupora mali, kwani waliposhuka wakateremka na kumkamata mfanyakazi ambaye alikuwa zamu siku hiyo,” alisema.

Kamanda Matei alisema kwamba baada ya kumkamata mfanyakazi aliyekuwa zamu ajulikanaye kwa jina la Samson Rufunga (33), pia wakaenda kumkamata na  mlinzi wa kituo hicho  aliyejulikana kwa jina la Mohamed Shaban (47).

Matei aliongeza kuwa baada ya kuwafunga kamba  za miguuni na mikononi waliwachukua wote wawili na kuwapeleka  katika chumba kimoja kilichpo katika kituo hicho na  kisha kuwafungia ndani.

Akifafanua zaidi kamanda huyo alibainisha kuwa majambazi hayo mbali na kuwateka wafanyakazi wa kituo hicho pia walimkamata Frank Nyamahaga (28), mkazi wa Tabata ambaye walimpora sh 100,000.

Mbali na kumpora fedha hizo pia walimchukulia funguo zake za  gari  aina ya Scania, ambalo lilikuwa limeegeshwa katika kituo hicho cha mafuta pamoja na kumpora simu zake mbili za mkononi aina ya Nokia zenye thamani ya sh 120,000.

Mwingine aliyeporwa vitu ni Isaac Silinu (25), utingo wa Scania hiyo, mkazi wa Ipogoro, Iringa ambaye naye aliporwa simu wakati Shabani Ramadhani (42)  mkazi wa Mwembetogwa, Iringa naye aliporwa simu.

Watu wengine walioporwa katika kituo hicho ni Issa Mohamed (25) mfanyabiashara,  mkazi wa Frelimo Iringa, ambaye aliporwa simu na sh 68,000.

Aidha, dereva wa pikipiki, Juma Selemani (30) mkazi wa Mwanalugali ambaye alikwenda kituoni hapo kwa ajili ya kujaza mafuta, naye aliporwa pikipiki yake aina ya SANLG na sh 4,600.

No comments:

Post a Comment