Pages

Monday, August 26, 2013

Mbagala Kuu watahadharishwa na matapeli

MBUNGE wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile (CCM), amewatahadharisha wakazi wa Mbagala Kuu kuepukana na watu wanaopita katika maeneo yao na kuchangisha sh 1,000 kwa kila mkazi kwa madai watawasaidia kupata haki zao juu ya fidia ya mabomu.

Ndugulile alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na wakazi wa mtaa wa Kichemchem, Kata ya Mbagala Kuu, Dar es Salaam na kusema watu hao wanafanya utapeli wa dhahiri kwa watu wenye matatizo.

Alisema zoezi la uthamini wa ulipaji fidia kwa wahanga wa mabomu ya Mbagala limemalizika na kwamba wale waliofanyiwa tathmini na majina yao yakashindwa kuonekana katika kumbukumbu za malipo wanapaswa wawasiliane na ofisi ya mbunge kwa hatua zaidi. “Vipo vikundi vinapita na kusema wapo karibu na Waziri Mkuu mara Rais, nawaambieni hao ni matapeli hakuna uthamini mwingine baada ya ule wa mwisho kumalizika,” alisema Ndugulile.

Kuhusu ulinzi mbunge huyo alisema ni wajibu wa kila mwananchi kukataa uhalifu na kuwafichua popote walipo badala ya kusubiri vyombo vya dola kufanya kazi hiyo.

“Kuna vijana 600 wanapata mafunzo ya polisi jamii; hawa watakuwa na mafunzo ya ukamataji salama pamoja na utunzaji wa mazingira, muwape ushirikiano watakaporejea kufanya kazi,” alisema Ndugulile.

No comments:

Post a Comment