Pages

Wednesday, August 7, 2013

Simba SC yakabidhiwa fedha za Mwinyi Kazimoto.


Mwakilishi wa Kamati ya Usajili ya Simba, Hans Pope (kushoto) akiwa na Mwakilishi wa Al-Markhiya Sports Club, Saleh Afif wakati akisaini fomu za usajili wa Mwinyi Kazimoto.


KLABU ya Simba imemuuza kiungo wake mshambuliaji, Mwinyi Kazimoto, katika timu ya Al-Markhiya Sports Club ya Qatar kwa dau la dola 50,000 (zaidi ya shilingi milioni 81) ambazo zaidi ya nusu zimeshakabidhiwa.

Kiungo huyo, hivi karibuni alitimkia huko kwa ajili ya kufanya majaribio kabla ya kusajiliwa na timu hiyo.

Akizungumza na Championi Jumatano katika makabidhiano ya fedha hizo, Mwakilishi wa Al-Markhiya Sports Club, Saleh Afif, alisema wametanguliza dola 35,000 (shilingi milioni 57).

Afif alisema fedha nyingine ambazo ni dola 15,000 (zaidi ya shilingi milioni 24) watazilipa mwishoni mwa Desemba, mwaka huu.

Alisema staa huyo akiwa kwenye timu hiyo, anatarajiwa kulipwa mshahara wa dola 7,000 (zaidi ya shilingi milioni 11).

Mwakilishi huyo alisema kiungo huyo amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini huko.

“Kazimoto amesaini kuichezea Al-Markhiya Sports Club ya Qatar kwa dau la dola 50,000 ambazo sehemu yake  tayari leo (Jumatatu) tumezikabidhi kwa mwenyekiti wao wa usajili, Hans Pope.

“Tumetanguliza fedha nyingine ambapo dola 15,000 tutazilipa mwishoni mwa Desemba, mwaka huu.  Akiwa kwenye timu hiyo anatarajiwa kulipwa mshahara wa dola 7,000,” alisema Afif.

Naye Hans Pope baada ya makabidhiano alisema kuwa wamemruhusu kiungo huyo kwenda kuichezea timu hiyo.

Hans Pope alisema hawawezi kumzuia kiungo huyo kwenda kucheza soka nje ya nchi, pia ameitaka timu hiyo kutorudia kitendo walichokifanya cha kumtorosha kambini Kazimoto na kumpeleka huko Qatar kwenye majaribio.

“Sisi hatuwezi kumzuia mchezaji yeyote kwenda kucheza soka nje ya nchi, kikubwa kinachotakiwa ni timu kufuata taratibu na siyo mlivyofanya kwa Kazimoto, kumtorosha kwenye kambi ya Stars na kumpeleka huko Qatar kwenye majaribio,” alisema Hans Pope.

No comments:

Post a Comment