Pages

Sunday, September 8, 2013

Jela kwa kumuweka kinyumba mwanafunzi...ni Amani Malilo DEREVA UNHCR - Katavi.

DEREVA wa Shirika la Kimataifa linalo hudumia wakimbizi (UNHCR)  katika  Mkoa wa Katavi, Amani  Malilo, amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela  baada ya kupatikana na hatia ya kuishi na msichana mwenye umri  wa miaka 16.

Msichana huyo ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Mishamo, wilayani Mpanda, Mkoa wa Katavi. Hukumu hiyo  ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi  Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Chiganga Ntengwa,  baada ya kuridhika na  ushahidi wa upande wa mashitaka.

Awali katika kesi hiyo, Mwendesha Mashitaka,  Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Razalo Masembo, aliileza mahakama kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo  Novemba 27 na Desemba 25, mwaka jana.

Ilidaiwa kuwa baada ya kumtorosha msichana huyo alisafiri naye hadi   wilayani Kasulu, mkoani Kigoma  na baada ya kutoka Kasulu alimhifadhi nyumbani kwake na kumuachia sh 5,000 kila siku kwa ajili ya chakula.

Mshitakiwa  inadaiwa waliendelea kuishi na kulala pamoja  na msichana huyo kwa kipindi chote hicho wazazi  wa binti huyo wakiwa wanaendelea kumtafuta  hadi  Machi 6, mwaka huu.

Inaelezwa kuwa siku hiyo, mtuhumiwa alisahau simu ndipo msichana huyo alipoichukua na kuitumia kumpigia mama yake kumjulisha mahala alipo.
 
“Baada ya wazazi kufikishiwa taarifa hizo  walilazimika  kwenda Kituo cha Polisi  cha Mpanda mjini  na siku hiyo hiyo  ya tarehe 26 Machi  mwaka huu  mnamo majira ya saa tisa  usiku  polisi walifika nyumbani kwa mshitakiwa  katika Mtaa wa Mji Mwema mjini hapa  na kumkuta mwanafunzi huyo  akiwa ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi  na mshitakiwa Amani,” alisema.

No comments:

Post a Comment