Pages

Monday, September 9, 2013

Mama Shujaa wa Chakula 2013 atimiza ndoto

MSHINDI wa shindano la Mama Shujaa wa Chakula, Sista Martha Mwasu, ameelezea kufurahia kutimiza ndoto yake ya kufungua kituo cha mafunzo ya ujasiriamali.
Kituo hicho kilichowezeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Oxfam, kinajulikana kama, Kituo cha Mama Shujaa wa Chakula 2013.

Sista Mwasu aliyeibuka kidedea katika shindano la Maisha Plus 2013, alibainisha hayo wakati wa uzinduzi wa kituo hicho kilichoko Kingolwira, mkoani Morogoro juzi.
Alisema akiwa mtawa wa kujitegemea, miaka mingi alikuwa na ndoto ya kumiliki ardhi, ili aweze kushirikiana na jamii katika shughuli za kijasiriamali, hususan kilimo na ufugaji.

“Tulipokuwa katika kijiji cha Maisha Plus, mlikuwa mnatuuliza tukishinda tunataka tuzawadiwe nini, mimi nilisema shamba, sasa leo hii namshuku Mungu, ndoto yangu ya muda mrefu imetimia,” alisema Sista Mwasu, ambaye awali alikuwa akiishi Haubi Kondoa, alisema hadi sasa kituo kina vijana 12, ambao anawafundisha namna ya kulima mazao mbalimbali katika eneo moja, hususan wakati wa kiangazi.

Aliyataja baadhi ya mazao yanayolimwa katika kituo hicho kuwa ni pamoja mahindi, alizeti, migomba, vitunguu, nyanya, uyoga, arovera, pilipili na hivi sasa wako kwenye majaribio ya tangawizi.

Mazao hayo baada ya kuvunwa, husindikwa kwa mitindo ya aina mbalimbali.
Akimwelezea Sista Mwasu, Ofisa Uhusiano wa Oxfam, Mwanahamis ... alisema, wakilima wanawake wanazalisha kati ya asilimia 60 hadi 80 ya chakula chote kinachotumika Tanzania, lakini wanamiliki asilimia 1 tu ya ardhi iliyosajiliwa, asilia 7 wanaofikiwa na huduma ya ughani na asilimia 10 wanaifikia huduma za kifedha.

“Katika muktadha huu Oxfam katika kampeni yake ya Grow imejikita katika kuhakikisha tunawekeza kwa wakulima wadogo wanawake ili kuwaongezea ari ya kuzalisha zaidi na kuondoa umaskini. Kituo hiki cha Mama Shujaa wa Chakula ambacho kimefadhiliwa na Oxfam na wadau wake wakiwemo NMB, kama zawadi ya mshindi wa kwanza, kinatarajiwa kuwa chachu ya kuwahamasisha vijana na kuwafikia kina mama wengi zaidi na kuwapa elimu ya uzalishaji bora bila kutumia kemikali na kutengeneza mfano wa jinsi gani wakulima wadogo wakiwezeshwa wanaweza kufanya mambo makubwa,” alisema Mwanahamisi.

Naye mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka, aliyemwakilisha Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, aliwapongeza waanzilishi wa shindano la Maisha Plus, Masoud Kipanya na Kaka Bonda, kwani wamebuni kitu cha Kitanzania na chenye faida kubwa kwa Watanzania na kuwataka wadhamini wazidi kuwaunga mkono.

“Tumekuwa tukishuhudia yakianzishwa mashindano mbalimbali lakini yasiyo na utamaduni wa kwetu, tumeona umiss wa kila aina, pia hata muziki wetu wa dansi ni wa kuiga, lakini kwa Maisha Plus ni kitu chetu na kina manufaa katika jamii,” alisema Mtaka.
Mtaka, pia alimpongeza Sista Martha kwa kujitolea kwake na kwamba amempa hamasa ya kwenda kuhamasisha wilayani kwake.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali akiwamo Mkurugenzi wa Oxfam Tanzania, Jane Foster, Mshindi wa Maisha Plus 2013, Bereniki Kimio ‘Mama Kevi’, mshindi wa pili Venance na washiriki wa Mama Shujaa wa Chakula, Theresia Kaseko wa Shinyanga, Tatu Abdi wa Lushoto Tanga na Mary Kawaka ‘Dogo’ wa Rukwa.
CHANZO TANZANIA DAIMA.

No comments:

Post a Comment