Pages

Friday, September 13, 2013

Mkenya aliyetimuliwa na wazee Yanga aula • Kiingilio mechi yao Mbeya City buku tano

UONGOZI wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, umemteua Mkenya Patrick Naggi, kuingia ndani ya sekretarieti ya klabu hiyo.

Naggi, alitua nchini takriban wiki moja iliyopita kuibua mtafaruku Jangwani, baada ya kudaiwa amekuja kurithi nafasi ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo, iliyokuwa ikikaimiwa na Lawrence Mwalusako, ambapo Katibu wa Baraza la Wazee la klabu hiyo, Ibrahim Akilimali, aliongoza mashambulizi ya kumtimua klabuni hapo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clemence Sanga alisema klabu yao ina upungufu mkubwa katika sekta mbalimbali, jambo lililowafanya kuongeza watu katika sekretarieti ili waje kusaidiana majukumu na waliokuwapo awali.
Sanga alisema mbali na Naggi, pia wamemuongeza George Simba na Salvatory Njovu, ambaye atakuwa kama mshauri ndani ya klabu hiyo.

Alisema watu hao walioongezwa hawana wadhifa wowote, hadi baada ya miezi miwili au kabla ndipo zitakapotangazwa nafasi zao.

“Hawa ni miongoni mwa viongozi wetu katika sekretarieti na baada ya miezi miwili au kabla tutatangaza nani anashika wadhifa gani na nani anafanya nini,” alisema Sanga na kuibua vicheko kwa waandishi wa habari waliokuwapo makao makuu ya klabu hiyo.

Licha ya viongozi wa Yanga kuonekana kusigina katiba yao ibara ya 37(1) inayosema kiongozi wa Sekretarieti anatakiwa kuwa mwanachama wa klabu hiyo, Sanga alisema suala hilo halina shaka kabisa na sasa wako mbioni kuwakamilishia kadi zao za uanachama.


“Suala la uanachama ni dogo sana, na sisi viongozi takriban kwa mwezi tunasajili zaidi ya kadi 100, hivyo basi hata hawa kadi watakuwa nazo siku si nyingi, kwani ni wapenzi wakubwa wa Yanga,” alisema Sanga.

Aliongeza kuwa, bado mchakato wa kumsaka Katibu Mkuu mpya wa klabu hiyo unaendelea kufanywa na kampuni ambayo wameingia nayo ubia, kwa ajili ya kufanikisha suala hilo.
Katika hatua nyingine, kuelekea mechi ya Yanga na Mbeya City kesho, Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (MREFA), kimewaonya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakifika kwenye Uwanja wa Sokoine kwa kutaka kuingia bure kushuhudia michezo mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom inayo endelea.

Mbali na kupiga ‘mkwara’ huo, chama hicho kimewataka wapenzi na mashabiki wa soka kukata tiketi katika vituo husika ambavyo vimetagazwa ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa chama hicho, Selemani Haroub, alisema ili kuwapunguzia mashabiki usumbufu, wametenga maeneo ya Uyole, Sae, Iyunga, Kabwe, Mwanjelwa, Uhindini na Uwanja wa Sokoine, ambako kutokana na hali ya uwanja huo kiingilio kitakuwa kimoja tu cha sh 5,000.

Mbali na hilo, katibu huyo alibainisha kuwa kutokana na ukubwa wa mchezo huo wameomba kibali Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Barabara ya Jamatini kutumika kama sehemu ya maegesho ya magari kuanzia saa saba mchana.

Aliongeza kuwa, utaratibu uliowekwa ni magari sita tu ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya uwanja.

Aliongeza kuwa maandalizi ya mchezo huo ambao Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, yamekamilika kwa asilimia 100 na kwamba, Yanga imeishawasili na inatumia uwanja wa Sekondari ya Wavulana Iyunga kwa ajili ya mazoezi.
Mchezo huo unazikutanisha timu hizo kwa mara ya kwanza katika historia ya soka ya Tanzania. Mbeya City imepanda Ligi Kuu msimu huu na Yanga ni mabingwa mara 23.

No comments:

Post a Comment