Pages

Thursday, September 19, 2013

Simba yapigiwa saluti sita Dar

KINYANG’ANYIRO cha Ligi Kuu ya Vodacom kiliendelea jana kwenye viwanja mbalimbali nchini, huku ikishuhudiwa Simba ya jijini Dar es Salaam ikiwafanyia mauaji maafande wa Mgambo JKT ya Tanga kwa kuipa kichapo cha mabao 6-0.

Wakati Simba ikitakata kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, watani zao Yanga jinamizi la sare liliendelea kuwaandama kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, baada ya kutoka sare ya 1-1 na wenyeji, Tanzania Prisons.

Jijini Dar es Salaam, Simba ilianza pambano kwa kasi na dakika ya pili tu, Amis Tambwe nusura aipatie bao baada ya shuti lake ndani ya boksi kupaa sentimita chache, kabla ya kurekebisha makosa dakika ya tano na kufunga bao maridadi kwa kichwa akiunganisha krosi ya Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.

Dakika ya 34, Simba ilipata bao la pili likifungwa na chipukizi Haruna Chanongo baada ya kuwalamba chenga mabeki na kipa Kulwa Manzi kutokana na shambulizi la pamoja kati yake na Tambwe.

Bao hilo, lilikuja dakika tatu tu tangu Betram Mwombeki aliposhindwa kuitendea haki krosi safi ya Chanongo wakati kipa akiwa amekwishapotea langoni.
Dakika ya 24, Tambwe alipachika bao la tatu akitumia vema udhaifu wa Manzi kudaka mpira kisha kumponyoka, kabla ya dakika ya 44, kukandamiza la nne, likiwa la tatu kwake katika mechi hiyo.

Hadi dakika 45 zinakamilika, Simba ilitoka uwanjani ikiongoza 4-0 huku ikiwa imetawala kipindi cha kwanza kwa asilimia kubwa.

Kutokana na mabao hayo ya kipindi cha kwanza, Kocha Mohamed Kampira wa Mgambo, alilazimika kumtoa kipa Manzi na kumuingiza Tony Kavishe.

Licha ya Mgambo kutawala dakika za mwanzo kipindi cha pili na kushindwa kuzitumia nafasi za kufunga dakika ya 49 na 58 kupitia kwa Salim Amlima na Bashiru Chanache, ilijikuta ikipachikwa bao la tano dakika ya 65 baada ya shuti kali la Chanongo kumbabatiza beki Bakari Mtama na kumpoteza kipa wake.

Dakika ya 76, Tambwe alihitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la sita kwa penalti, baada ya Peter Mwalianzi kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Hadi mwamuzi Jacob Adongo wa Mara aliyekuwa akisaidiwa na Ferdnand Chacha, Grace Wamara kutoka Kagera, akiashiria dakika 90 kukamilika, Simba 6, Mgambo 0.
Simba: Abel Dhaira, Miraji Adam/William Lucian, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Henry Joseph/Ramdhani Chombo ‘Redondo’, 
Betram Mwombeki/Twaha Ibrahim, Amis Tambwe, Haruna Chanongo.

Mgambo JKT: Kulwa Manzi/Kavishe, Francis Anyosisye, Salum Mlima, Bakari Mtama, Novat Lufunga/Bashiru Chanache, Salum Kipaga, Nassoro Gumbo, Peter Mwalianzi, Mohamed Neto, Fully Maganga, Salum Gilla.

Kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, wenyeji Azam FC walilazimishwa sare ya bao 1-1 na vibonde wanaoburuza mkia, Ashanti United.

Jijini Mbeya, mabingwa watetezi Yanga licha ya kutangulia kujipatia bao dakika ya 43 likifungwa na Jerry Tegete kwa kifua akiunganisha krosi ya Simon Msuva ilijikuta ikimaliza mchezo kwa sare ya 1-1.

Prisons ilisawazisha dakika ya 72, kwa bao la Peter Michael akiitendea haki kona ya mchezaji aliyetokea Yanga msimu uliopita, Omega Seme. Hii ni sare ya pili mfululizo kwa Yanga. Jumamosi iliyopita ililazimisha sare ya 1-1 kwa Mbeya City kwenye uwanja huo wa Sokoine.

Prisons: Beno David, Salumu Kimenya, Mika Shaban, Juma Elfadhil, Nurdin Issa, Lugano Mwangama, Jimy Shoji, Fredy Chudu, Ibrahim Issake, Six Ally, Jeremia Juma, Subu Ibrahimu, Beniphese Hau, Julius Uwage, Peter Michael, John Esen, Omega Seme, Hamis Rajab.

Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Lihende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Athuman Idd ‘Chuji’, Simon Msuva, Salum Telela, Didier Kavumbagu, Jerry Tegete, Haruna Niyonzima.

Kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi, mkoani Pwani, waliokuwa vinara wa Ligi, JKT Ruvu walitulizwa na ndugu zao Ruvu Shooting, baada ya kukubali kulala kwa bao 1-0, mfungaji akiwa Stephano Mwasika.

Jijini Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani, wenyeji Coastal Union walitoka sare ya bao 1-1 na Rhino ya Tabora, wakati huko Manungu, Turiani Morogoro, Mtibwa ililazimishwa sare ya bila kufungana na Mbeya City.

Kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba mkoani Kagera, wenyeji Kagera Sugar walikwenda sare ya 1-1 na JKT Oljoro ya Arusha.
Kwa matokeo ya mechi hizo za mzunguko wa nne, Simba imefanikiwa kukamata usukani wa ligi, ikifikisha pointi 10 na kuwashusha Ruvu JKT wenye pointi 9.

No comments:

Post a Comment