Pages

Thursday, September 19, 2013

Viingilio Redd’s Miss Tanzania vyatajwa..

WAKATI zikiwa zimebaki siku tatu Redd’s Miss Tanzania ajulikane, viingilio kwa ajili ya shindano hilo linalosubiriwa kwa hamu vimetangazwa.
 
Kiingilio cha juu katika shindano hilo linalotarajiwa kufanyika Jumamosi, ukumbi wa Mlimani City, Mwenge jijini Dar es Salaam ni sh 100,000 viti maalumu, huku vya kawaida vikiwa sh 50,000.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa kinywaji cha Redd’s Original, Victoria Kimaro, ambao ndio wadhamini wakuu wa Redd’s Miss Tanzania alisema, wanaamini viingilio hivyo ni vya kawaida kutokana na ubora wa shindano lenyewe.

Victoria alisema, burudani katika shindano hilo inatarajiwa kutolewa na msanii mahiri kutoka Uganda, Mike Ross atakayeshirikiana na Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ pamoja na kundi la Mama Afrika katika kukonga nyoyo za mashabiki watakaojitokeza ukumbini hapo.

“Tunaamini kabisa wasanii hawa watakonga nyoyo za mashabiki wa tasnia ya urembo hapa nchini, hivyo napenda kutoa wito kwa mashabiki kujinunulia tiketi mapema ili kuepuka usumbufu,” alisema Victoria.

Naye Lady Jaydee alisema, kwa kushirikiana na bendi yake ya Machozi, wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa burudani ya nguvu kwa mashabiki wote watakaohudhuria.

“Nawaomba mashabiki wangu na wale urembo, kujitokeza kwa wingi ili kufurahia burudani nzuri toka kwangu na bendi yangu ya Machozi, pia wasanii wenzangu waalikwa naamini watafanya vizuri siku hiyo,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashimu Lundenga ambao ni waratibu wa Redd’s Miss Tanzania alisema, tiketi za shindano hilo tayari zimeishaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Alitaja maeneo ambayo yameteuliwa kuuza tiketi za Redd’s Miss Tanzania kwa mwaka huu ni duka la Shear Illusion lililopo Mlimani City, City Sports Lounge na Steers zilizopo Mtaa wa Samora, Faberk Fashion, Rose Garden Pub na ofisi za Redd’s Miss Tanzania ambazo zote zipo eneo la Mikocheni.

Lundenga alifafanua kuwa, ili kuwapa fursa watu wengi zaidi tiketi itakayonunuliwa katika vituo vilivyopangwa kabla ya shindano itakuwa ni Sh 80,000 na kutakuwa na ofa kadhaa.
Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Brigitte Alfred, aliyefanikiwa kulitwaa mwishoni mwa mwaka jana.

Shindano la Redd’s Miss Tanzania linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

No comments:

Post a Comment