Pages

Saturday, September 28, 2013

Wasichana 55,000 wakosa masomo kwa ujauzito.

ZAIDI ya wasichana 55,000 wa shule za msingi na sekondari Tanzania Bara, wamekatisha masomo yao kwa sababu za ujauzito.

Licha ya kukatisha masomo, wasichana hao walitengwa na jamii baada ya kupata ujauzito na kuwaharibia mtiririko bora wa maisha yao katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Hayo yalibainika Dar es Salaam juzi usiku wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti namna Wasichana wa shule nchini Tanzania wanavyofanyiwa kwa nguvu vipimo vya ujauzito na kufukuzwa wanapokutwa wajawazito.

Utafiti huo ulifanywa na Kituo cha Kutetea Haki ya Uzazi kiitwacho Centre for Reproductive Rights kati ya mwaka 2012/2013 na kubainisha hayo huku ukieleza kwamba asilimia 44 ya wasichana Tanzania Bara wamepata mimba wakiwa na umri chini ya miaka 19 huku wengi kati yao wakitengwa na jamii.

Akizungumzia utafiti huo mkurugenzi mkazi wa kituo hicho kanda ya Afrika Evelyne Opondo alisema utafiti huo umehusisha shule za bweni za serikali na binafsi.

“Tumegundua kwamba wakuu wa shule wanawapima mimba wananfunzi kwanza kwa njia za kienyeji, pili wanafanya hivyo bila kujua kwamba hakuna sheria wala sera inayowaruhusu kuwapima mimba wanafunzi hao.

“…Lakini wakuu wa shule na serikali za maeneo hayo wanafanya hivyo bila kujua hawaruhusiwi,” alisema Evelyne huku akisisitiza kwamba hakuna sheria inamwadhibu mtoto wa shule kwa kumzuia kuendelea na masomo huku ikiwa bubu kwa aliyemtia ujauzito huo.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Baraza la Afrika la Haki na Usawa wa Mtoto Dk. Clement Mashamba alisema hakuna utaratibu sahihi wa kisheria wa kumwajibisha aliyemtia ujauzito mwanafunzi huku akishauri kuwepo na mfumo mmoja wa kuwaadhibu wanaume hao.

No comments:

Post a Comment