Pages

Friday, September 13, 2013

Zawadi Redd’s Miss Tanzania hadharani...Malkia kuondoka na gari, mil. 8/-

MALIKIA wa taji la Redd’s Miss Tanzania 2013 anatarajiwa kuondoka na gari dogo lenye thamani ya sh milioni 15 sambamba na kitita cha sh milioni nane.

Shindano hilo linalotarajiwa kushirikisha warembo 30 kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini, limepangwa kufanyika Septemba 21, mwaka huu, kwenye ukumbi wa Mlimani City, huku likipambwa na burudani za kila aina kutoka kwa wasanii maarufu wa ndani na nje.

Akitangaza zawadi hizo jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa kinywaji cha Redd’s Original, Victoria Kimaro, alisema wameamua kutangaza mapema zawadi hizo ili kuleta morali kwa washiriki wa shindano hilo.

“Tunaamini shindano la mwaka huu litakuwa na ushindani mkubwa zaidi na zawadi hizi zitakidhi kwa kiasi kikubwa mahitaji ya warembo,” alisema Victoria.

Mbali na mshindi kutwaa zawadi hizo, mshindi wa pili atapata sh milioni 6.2, wa tatu sh milioni nne, wa nne sh milioni tatu, wa tano sh milioni mbili, huku mshindi wa sita hadi 15 watapata sh milioni 1.2 kila mmoja na waliobaki watajipoza kwa sh 700,000 kila mmoja.

“Thamani ya fedha taslimu itakuwa ni sh milioni 46.1 na zawadi zote hizi watakabidhiwa warembo wa Redd’s Miss Tanzania siku inayofuata baada ya kufanyika kwa fainali hizo,” alisema Victoria.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga, ambao ndio waandaaji, aliwashukuru wadhamini na kusema, wamefanya kazi kubwa zaidi katika kuyakuza mashindano hayo.

“Kwa mara nyingine tunapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wadhamini wetu wakuu Redd’s Original na wadhamini wenza, ambao kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha shindano la mwaka huu linakuwa zuri zaidi,” alisema Lundenga.

Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Brigitte Alfred, aliyelitwaa taji hilo mwaka jana na kukabidhiwa gari aina ya Noah, pamoja na kitita cha sh milioni nane.
Shindano la Redd’s Miss Tanzania linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original.

No comments:

Post a Comment