Pages

Saturday, October 19, 2013

‘Fedha za misaada zaishia mifukoni’

UFISADI uliokithiri katika fedha za misaada zinazotolewa na serikali kusaidia wajasirimali umekuwa kikwazo kwa Watanzania kujiendesha.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkuu wa Chuo cha Ufundi Mtakatifu Gaspar kilichopo Kunduchi, Achileus Mutalemwa katika mahafali ya chuo hicho.

Alisema fedha za misaada zimekuwa haziwafikii walengwa, hivyo kuishauri serikali kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha inapotoa fedha zinawafika walengwa.

“Tunakumbuka kuna mabilioni yalitolewa kwa wajasiriamali, lakini ni wachache waliopata, lakini fedha nyingi zilichukuliwa na mafisadi,” alisema.

Alisema chuo hicho kinazalisha bidhaa zenye ubora na zinazofaa kununuliwa na serikali kutokana na uimara na kutumia mbao za hapa nchini.

Mkuu huyo wa chuo alisema ni muhimu serikali kuweka mkazo kwa viwanda vya ndani, hasa wajasiriamali wadogo ambao wamekuwa wakizalisha kwa kutumia nguvu nyingi, lakini mauzo yake yanakuwa hafifu.

“Hapa kwetu tunafundisha useremala, mapishi na hata udereva, na vijana wamekuwa wakifanya vyema katika uzalishaji wa bidhaa, kinachotukwamisha ni kitendo cha kuingizwa kwa bidhaa za nje ambazo hazina ubora, lakini zinauzwa kwa bei ya juu,” alisema.

No comments:

Post a Comment