Pages

Friday, October 18, 2013

Halmashauri Bagamoyo lawamani.

WAKAZI wa vijiji vitatu katika Halmashauri ya Bagamoyo, Pwani wameilalamikia halmashauri hiyo kwa kumkumbatia mwekezaji na kuchukua ardhi huku wakiambulia malipo kidogo.

Wakizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni waliotembelea vijiji hivyo, wanakijiji hao walimtaja mwekezaji huyo kuwa ni Subash Patel, ambaye amechukua eneo hilo kwa makubaliano ya kuwalipa sh 700,000 kwa ekari moja.

Walidai mwekezaji huyo alichukua ardhi yenye ukubwa wa ekari 8,500 atakazotumia kujenga kiwanda cha saruji.

Mtendaji wa Kijiji cha Magulumatala, Masudi Ali, alisema malipo yaliyotolewa na mwakilishi wa Patel ni kidogo tofauti na makubaliano ya awali.

“Nimeshuhudia mtu akilipwa sh 12,000, ni kiasi kidogo ukilinganisha na thamani halisi ya ardhi ilivyo hivi sasa katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema.

Naye Shabani Masudi, alidai mwekezaji huyo amekiuka makubaliano na inaashiria kuwa kuna dhuluma kutokana na kiasi kidogo kilicholipwa.

“Baadhi ya kasoro tunazolalamikia ni kupunjwa malipo, kupunjwa ukubwa wa maeneo mbalimbali yaliyofanyiwa tathmini na hata wanakijiji wengine wameshindwa kuona majina yao,” alisema.

Alivitaja vijiji vilivyoathirika na zoezi hilo ni Mkenge, Tulawanda na Magukumatala.
Akijibu tuhuma hizo, msemaji wa mwekezaji huyo, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa MMi Steel Ltd, inayotaka kuwekeza katika eneo hilo, Abubakary Mlawa, alisema hakuna ukweli katika suala hilo bali halmashauri ndiyo iliyofanya tathmini ya maeneo hayo na wala si mwekezaji.

Mlawa alisema katika kikao chao na halmashauri, wanavijiji hao walikubaliana kulipwa sh 400,000 kwa ekari na kulipia mazao yaliyokuwepo, jambo ambalo limetekelezwa na kampuni hiyo.

“Yaani kama wanadai malipo ni madogo basi watakuwa wamedhulumiana wao wenyewe na si sisi kama wanavyodai maana hata ukiangalia gharama za eneo hilo kabla ya mwekezaji kuhitaji walikuwa wakiuza sh 200,000 lakini waliposikia tunayahitaji ndipo walipotupandishia bei,” alisema.

No comments:

Post a Comment