Pages

Friday, October 18, 2013

KCB yakabidhi madawati 700.

BENKI ya KCB imesema inatambua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini na kuahidi kuendelea kuwekeza kwa ajili ya kuinua kiwango cha elimu nchini.

Mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Dk. Edmund Mndolwa, alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana alipokabidhi madawati 700 katika shule saba za serikali jijini Dar es Salaam.

Alisema benki yake inatambua matatizo mbalimbali yanayoikabili sekta ya elimu nchini, hivyo wataendelea kusaidia kulingana na kile wanachokipata.

“Leo tunahitimisha kampeni ya nunua madwati 10 upate mengine 90 ambayo imehusisha shule za serikali jijini hapa, sita zikiwa za msingi na moja ya sekondari, ambayo lengo lake kuu ni kuboresha mazingira ya elimu,” alisema Mndolwa.

Mkuu wa kitengo cha masoko na mawasiliano wa benki hiyo, Christina Manyenye, alisema thamani halisi ya madawati yote ni sh milioni 121 na kwamba KCB ilichangia zaidi ya sh milioni 114 huku shule husika zikichangia sh milioni saba.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbuyuni, Doreen Malecela, aliishukuru KCB kwa kuchangia madawati hayo ambayo yataongeza ari ya kusoma shuleni hapo.

Miongoni mwa shule zilizonufaika na kampeni hiyo iliyodumu kwa mwezi mmoja ni Mbuyuni, Makumbusho, Sinza, Mkunguni, Msasani B, Hananasif na Shule ya Sekondari Oysterbay.

No comments:

Post a Comment