Pages

Thursday, October 10, 2013

Mgomo wanukia Simba..Henry Joseph atoswa kambini.

WACHEZAJI wa Simba wakiwa kwenye mgomo baridi kushinikiza kuondolewa kwa Kocha Msaidizi Jamhuri Kihwelo ‘Julio,’ kiungo Henry Joseph ametemwa kwenye kikosi cha timu hiyo kilichoingia kambini Bamba Beach, juzi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kujiandaa na mechi za Ligi Kuu.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema kuwa, chanzo cha kuachwa kwa Henry ni baada ya kusigana na Julio tangu Jumatatu wiki hii wakati wa mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi, ambapo nyota huyo aligomea mazoezi.

Kuna habari kuwa, Henry alipoulizwa ni kwanini alikuwa kwenye hali ya kusuasua, akajibu kuwa tayari alishajifua kivyake, jibu ambalo lilimkera Julio na kumtaka aondoke uwanjani hapo, hivyo kutojumuishwa kambini.

Tanzania Daima ilipojaribu kutafuta kiini cha msigano ndani ya timu hiyo, baadhi ya wachezaji walikiri Henry kusigana na Julio na kuongeza kuwa, kuna mgomo baridi unaotokana na wao kukerwa na kocha huyo msaidizi.

Chanzo hicho kilidokeza kuwa, Julio amekuwa akichukiwa na wachezaji kutokana na lugha zake za karaha na matusi, ambazo zimekuwa zikiwanyima raha wachezaji dimbani hasa kwenye mazoezi.

“Hali sio nzuri katika timu yetu, mpaka sasa Henry hayupo kambini baada ya kutokea mabishano baina yake na Julio, tukiwa mazoezini Jumatatu,” alisema mmoja wa wachezaji wa timu hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, alisema hajui lolote kuhusu suala hilo na kama kuna ukweli, bado ni suala la kiutendaji zaidi linalohitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi kabla ya kutolewa majibu kwa maslahi ya Simba.

Juhudi za kumpata Julio kutoa ufafanuzi wa kilichotokea kati yake na Henry, ziligonga mwamba kwani licha ya kutafutwa mara kadhaa kwa siku ya jana, simu yake haikuwa hewani.CHANZO NI TANZANIA DAIMA.

No comments:

Post a Comment