Pages

Tuesday, October 1, 2013

Ruguluni haina shule miaka 14

MWENYEKITI Serikali ya Mtaa Ruguluni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Saidi Mahadula, amesema mtaa huo haujawahi kuwa na shule ya msingi tangu ulipoanzishwa miaka 14 iliyopita.
Mahadula alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa hadhara uliokuwa ukijadili maendeleo na kero za mtaa huo, uliofanyika kwenye viwanja vya Dk. Halid, Makondeko.

Alisema kutokana na kukosekana kwa shule katika mtaa huo, watoto hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata shule, jambo ambalo wakati mwingine ni hatari kutokana na baadhi yao kuwa na umri mdogo.

Aliyataja maeneo ambayo watoto hao wamekuwa wakifuata shule kuwa ni Mbezi Luis, Kibamba, Mpijimagohe na Mshikamano.
“Umefika wakati wa kuunganisha nguvu zetu na tushirikiane, ili kwa pamoja tuweze kumaliza kero inayotukabili,” alisema Mahadula.

Ili kumaliza kero hiyo, wakazi hao kwa pamoja wamekubaliana kuanzisha mchakato wa kujenga shule kwa kuanzisha kitu walichokiita ‘Dira ya Maendeleo’.

Mahadula alisema lengo la dira hiyo ni kutafuta fedha kutoka manispaa ya Kinondoni, Serikali Kuu, wafadhili wa ndani na nje ya nchi, kampuni za simu, wadau mbalimbali na wakazi wa mtaa huo ili kufanikisha azma hiyo.

No comments:

Post a Comment