Pages

Saturday, April 26, 2014

BABA AHUSISHWA KIFO CHA DENTI MWANZA!

Mwili wa marehemu Anastazia Lackfordukiagwa kabla ya kwenda kuzikwa.
Mwili wa marehemu Anastazia Lackford ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwanza, umezikwa juzi katika makaburi ya Lunala, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza lakini simulizi ya baba mzazi wa marehemu, Lackford Magafu kuhusishwa na kifo cha mwanaye inashangaza!
Kabla ya kifo.

Mwili wa marehemu Anastazia Lackfordukiwa kwenye jeneza
Inadaiwa kuwa, Machi 27, mwaka huu baba wa marehemu, Magafu alimpiga sana mtoto huyo kwa madai ya kutopika chakula kwa wakati.
Ilizidi kudaiwa kuwa, mbali na kipigo hicho mzazi huyo alimmwagia mafuta ya taa na kumchoma moto, hali iliyomsababishia majeraha mwilini.
“Baada ya ukatili huo, baba huyo alimchukua Anastazia na kwenda naye Kituo cha Polisi cha Igogo ambako alidanganya kuwa, mwanaye alilipukiwa na jiko, uongo ambao marehemu aliukubali ili kumuokoa baba yake,” kilidai chanzo kilichoomba hifadhi ya jina lake.
Ikaelezwa kuwa, mtoto huyo alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Butimba, baadaye Sekou Toure kabla ya kupelekwa Bugando na kulazwa wodi ya wagonjwa mahututi, wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).
Chanzo cha kifo
Hata hivyo, kifo cha Anastazia kilichotokea Aprili 16, mwaka huu hakijathibitishwa kimesababishwa na majeraha yaliyotokana na moto au kinachodaiwa kuwa ni sumu iliyowekwa kwenye juisi inayodaiwa kupelekwa na Magafu wakati marehemu alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Bugando.
Mmoja wa watu waliokuwa wakimuuguza Anastazia (jina linahifadhiwa) alidai kuwa, siku hiyo Magafu alipeleka juisi hiyo na baada ya mgonjwa kuinywa alianza kujisikia vibaya.
Awali, Anastazia aligoma kuinywa juisi hiyo kana kwamba alihisi kitu lakini baada ya kulazimishwa aliinywa kwa shingo upande.
“Baba yake alipoondoka tu, Anastazia akaanza kujihisi vibaya, akawa anatapika mabonge mabonge ya vitu vyeusi.
“Nilipompigia simu baba yake na kumwambia hali ya mgonjwa na kumuuliza kama juisi ile alitengeneza mwenyewe, amenunua au amepewa, alinijibu kuwa ametengeneza yeye.
“Akaniambia nisimwambie mtu lakini nikaona ni bora kuwaambie ndugu zake na wauguzi, haikuchukua muda mrefu mgonjwa akawa amefariki,” alidai mtoa habari huyo bila kueleza chanzo hasa cha kifo hicho.
Akizungumzia kifo cha mwanaye, mama mdogo wa marehemu, Nongwa Gilbert alisema hana cha kusema bali anamwachia Mungu.
“Nimeshazungumza sana hadi nimechoka, kilichobaki namwachia Mungu maana hata nikizungumza sitaweza kumrudisha,” alisema Nongwa.
Hadi sasa Magafu anashikiliwa na jeshi la polisi jijini Mwanza na kuhusu juisi aliyopewa Anastazia kusababisha kifo chake, Kamanda wa Polisi Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Valentino Mulowola alisema:
“Uchunguzi ulifanyika, lakini majibu bado yanasubiriwa kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye amepelekewa sampuli kwa uchunguzi wa kisayansi. Suala la mtuhumiwa kufikishwa mahakamani ni uamuzi wa Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP).”
Marehemu alizaliwa Januari 30,1997, alisoma Shule ya Msingi Kirumba kuanzia mwaka 2004, akajiunga Shule ya Sekondari Mwanza mwaka 2011. Hadi anafariki dunia alikuwa kidato cha tatu akichukua masomo ya sanaa.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi-Amin.

No comments:

Post a Comment