Stori: Shani Ramadhani
Mama mmoja, Sara Zoya
mkazi wa Mabibo Makuburi, jijini Dar es Salaam amekimbilia polisi na
kudai kuwa watoto wake walitekwa na ndugu yake kisha kupelekwa
kusikojulikana baada ya kufukuzwa kwenye nyumba yao ya familia.
Sara alidai kuwa ndugu yao huyo aliyefanya kitendo hicho cha utekaji
ni Hilda Zoya ambaye anadai aliwateka watoto Imani (14) na Leila (5).
Akizungumza na gazeti hili Sara alisema, alikuwa akiishi na mumewe na
baada ya kuachika kwa mume wake aliamua kurudi kwao kwenye nyumba ya
familia na watoto hao wawili. Aliendelea kufafanua:
“Sisi tulizaliwa watoto sita kwa baba na mama mmoja na mimi ndiye
mtoto wa kwanza na wazazi wetu wote walishafariki dunia. Mimi
nilipoachika niliwataarifu ndugu zangu kuwa nataka kurudi nyumbani
kwetu Mabibo lakini baadhi yao wakanishauri niende nikakae Tabata
Kisukuru kwenye nyumba ya mdogo wangu anayeishi Ulaya.
“Mimi sikupenda, nikakataa nikaenda kuishi kwetu, ilipofika Desemba
17 mwaka huu, ndugu yangu Rachel kutoka Ulaya aliyekuja likizo aliniomba
nimsindikize kwa mjomba anayeishi Mbezi Beach huku nyuma mdogo wangu
Hilda alihamisha vyombo vyote na kuwachukuwa watoto na kuwapeleka
kusikojulikana.
“Niliporudi nyumbani nilikuta milango imefungwa na vitasa vimebadilishwa na kuwekwa mlinzi pia watoto wangu wawili sikuwakuta.
“Nikaenda kwa mjumbe, mwenyekiti wa serikali za mitaa kuwaarifu na
baada ya hapo nikaenda kutoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi cha
Mwongozo kilichopo External, wakaniambia nisubiri kwa muda wa saa 24
lakini sikuwaona wanangu na mama yao mdogo Hilda alikuwa hapatikani
kwenye simu, ndipo nikaamua kurudi tena kituoni hapo na kufungua kesi
kuhusu kutoonekana kwa watoto, vitu vyangu na mimi kukosa pa kulala.”
Sara amemfungulia kesi mdogo wake Hilda kwa jalada namba
MWP/RB/1655/2014 UTEKAJI WA WATOTO NA WIZI hivyo anasakwa na
polisi.Akifafanua zaidi mama huyo alisema: “Siku ya pili watoto
walirudi wenyewe na walipohojiwa walidai walipelekwa Kinondoni kwa
Manyanya na mama yao mdogo na kutelekezwa huko na aliwaachia shilingi
elfu tano.
“Watoto walisema walipoamka asubuhi waliwauliza wapangaji wa nyumba
hiyo wapi walipo na wakaelekezwa kuwa pale ni Kinondoni kwa Manyanya.”
Mtoto Imani alipoulizwa na gazeti hili alikiri kuchukuliwa na mama
yao mdogo na kutelekezwa Kinondoni. “Asubuhi tuliwaomba wapangaji
watuelekeze namna ya kufika stendi, tukapelekwa tukapanda basi mpaka
Makumbusho kisha tukafika nyumbani, tukaelezwa kuwa mama alilala kwa
mwenyekiti wa serikali za mitaa.”
Sasa Sara anaomba msaada wa kisheria kwani alidai yeye pamoja na
watoto wake hawana nguo, vyombo na sehemu ya kuishi baada ya kufanyiwa
unyama huo na mdogo wake huyo na sasa wamefadhiliwa na mwenyekiti wa
serikali za mtaa wanakoishi.
No comments:
Post a Comment