HII ndiyo A-Z ya wale watu tisa wanaoshikiliwa na polisi jijini Dar
baada ya kukamatwa msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na
bendera nyeusi inayodaiwa kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab.
Mmoja kati ya watu hao (wa kumi), Hamad Makweka aliuawa.
Watu hao walikamatwa Aprili 14, mwaka huu saa 3:30 usiku katika
Kitongoji cha Nyandero Tarafa ya Kidatu wilayani Kilombero, Morogoro
wakiwa na silaha hizo ambapo ilidaiwa kuwa, walikuwa wakijiandaa kwenda
kufanya uhalifu wa ‘kigaidi’ mahali.
Ilidaiwa watu hao walilala kwenye Msikiti wa Answar Sunna uliopo Kidatu ambao unamilikiwa na Islamic Foundation.
Baada ya kukamatwa, awali walishikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi,
Morogoro na baadaye kupelekwa jijini Dar kwa siri ambako mahojiano
makali yanaendelea.
Habari kutoka ndani ya jeshi hilo zinasema kuwa, watu hao wanahojiwa
ili kujua ukubwa wa mtandao wao, walikuwa wakafanye tukio wapi na nani
mdhafili wao mkubwa.“Unajua kwa sasa tatizo ni kwamba, inaonekana
wahalifu wakubwa tunaishi nao, zamani tuliamini wanaweza kuingia kutoka
nje ya nchi.
“Wale jamaa walikuwa wakijiandaa kwenda kufanya uhalifu mahali, hilo
ni moja lazima waseme. Pia lazima mtandao wao ujulikane. Jeshi la polisi
lilifanya kazi yake kwa usahihi ndiyo maana walinaswa kabla ya muda wa
kwenda kufanya tukio,” alisema askari mmoja kwa kuomba jina lake
lisitumike kwa kuwa si msemaji wa jeshi hilo. Gazeti la Uwazi lilifika
kwenye Msikiti wa Suni na kuzungumza na baadhi ya watu. Mtu wa kwanza
kuongea naye alikuwa muumini wa msikiti huo, Shani Kinyimbi ambaye
alisema:
“Kwa hili lililotokea, mimi nawaomba viongozi wetu wa msikiti huu
kuanzia leo mtu asilale ndani na baada ya swala msikiti ufungwe. Hii ni
hatari sana, magaidi kugeuza msikiti sehemu ya maficho imeniuma sana
msikiti wetu kuchafuliwa.”
Naye kiongozi mmoja wa msikiti huo, Mohamed Menze ambaye ni mweka
hazina mkuu alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema:“Tukio hili la
kigaidi limeuchafua sana msikiti wetu na dini yetu kwa ujumla. Kiukweli
hawa jamaa sisi kama viongozi wa msikiti hatuwajui na wamefika usiku na
kukamatwa usiku huohuo.
“Hapa msikitini kuna vijana watatu wanalala ambao ni Hafidh Kondo,
Rajabu Shomari, Singo na Mustapha Kivale. Kwa mujibu wa vijana hao, juzi
(Aprili 14) usiku walifika watu hao wakiwa na mabegi ya kitalii na
kuswali ambapo baada ya kuswali waliomba kulala msikitini
“Wakati wakiendelea kuongea na vijana wetu polisi walifika na
kuwakamata na baadaye kwenda kwa imamu wetu ambao walimuuliza kama ana
taarifa za ugeni huo imamu alikana kuwa na taarifa, polisi waliwakamata
watuhumiwa hao na walipopekuliwa kwenye mabegi yao walikutwa na sare za
jeshi, bendera, baruti na vitu vingine mbalimbali. Wakati huo mwenzao
mmoja alishauawa.”
Diwani wa Kata ya Kidatu, Bryson Mwanzenye alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema:
“Hili ni tukio la kigaidi na kwa sasa kwenye kata yangu hali ni tete,
mtu mwenye ndevu nyingi na kipara (Hamad Makweka) ambaye hafahamiki
alivamiwa na kupigwa na wananchi wenye hasira hadi kufa.”
Alipotakiwa kueleza alivyomfahamu marehemu Hamad Makweka alisema:
“Huyo mtu si mkazi wa kata yangu, anatoka Ruaha lakini mtu anapokufa
ndipo mengi yanapoibuka. Inadaiwa huyo marehemu alikuwa ni mwalimu wa
kareti ambaye majirani zake wanasema hawakujua kazi yake lakini alikuwa
ni mtu wa kusafirisafiri sana.”
Maulidi Aliphonce ambaye ni dereva wa Bajaj ya pili iliyowachukua baadhi ya watu hao kwenda nao msikitini, alisema:
“Mimi niliwachukua watano kati ya wale watu kutoka kituo cha Ruaha.
Mwenzangu (Bajaj ya kwanza) aliwachukua watano. Tukiwa tunaenda
msikitini, kwa nyuma tulifuatwa na pikipiki mpaka tunafika msikitini.
“Nilipowashusha, ile pikipiki iligeuza na sisi wa Bajaj tukageuza
kurudi kituoni kwetu. Lakini mtu mmoja Hamad Makweka aligeuza na mimi
licha ya kwamba wakati wa kuwabeba wenzake na yeye alikuwemo lakini
alisema anarudi Kidato kwa sababu wenzake watalala msikitini.
“Njiani tukakutana na polisi, wakatusimamisha. Wakaanza kumuuliza
maswali Hamad, ghafla naye akatoka mbio, polisi mmoja akamkimbiza, Hamad
akatoa sime na kumkata shingoni yule askari na kutaka kuendelea
kukimbia, lakini polisi mwingine alimpiga risasi ya mguu, akaanguka na
kukamtwa.
“Ndipo wananchi wenye hasira kali walipotokea na kumpiga mpaka
wakamuua kwa kumchoma moto. Walimpiga kwa sababu alimkata shingo askari
kwa kuulizwa maswali kadhaa.” Naye Koplo Nassoro Dabi ambaye ni
mchezaji wa zamani wa Timu ya Polisi, Morogoro aliyekatwa shingo kwa
sime na marehemu Hamad ambaye kwa sasa amelazwa Zahanati ya Kikosi cha
Kutuliza Ghasia, Morogoro alikuwa na haya ya kusema:
“Namshukuru Mungu hadi leo hii napumua. Kwa kweli nilinusa kifo,
sikujua kama jamaa alikuwa na sime kiunoni. Wakati namfukuza aliingia
kwenye shimo na kuangua, nilipojiandaa kumkamata alitoa sime na kunikata
shingoni nikapoteza fahamu baada ya kutoka damu nyingi.
“Kama ningejua ana sime ningejua namna ya kumwingia. Lakini kwa kweli
ilikuwa hali tete pale. Ila wananchi wa kule wana umoja sana.”Siku za
hivi karibuni kumeibuka uhalifu wenye kutia shaka hasa kutokana na
silaha wanazokuwa nazo wahalifu hao kiasi kwamba, wapo waliobainika kuwa
na ushirika na Kundi la Kigaidi la Al Shabaab la nchini Somalia. Mfano
ni kijana Rashid Charles Mberesero (21) ambaye alihusishwa na mauaji ya
wanafunzi 148 kwenye Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya mapema mwezi
huu.
No comments:
Post a Comment