BINTI Muhadia Juma ambaye alikuwa mmoja wa watoto
watatu waliofungiwa ndani ya nyumba kwa miaka kumi na mama yao mzazi,
Mwasiti Ally katika Kijiji cha Kanga, wilayani Mafia amefariki dunia
Aprili 15, mwaka huu.Huyu ni kijana wa pili kufariki dunia baada ya
Ally Juma kuaga dunia hivi karibuni na kufanya aliyebaki hai kuwa mmoja,
Mzee Juma.
Muhadia alichukuliwa kijijini kwao na kupelekwa Hospitali ya Wilaya
ya Mafia kwa matibabu na mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Nassoro Hamid
aliyepata taarifa za kufungiwa ndani kwa miaka kumi na mama yao kupitia
gazeti hili toleo la Machi 31, mwaka huu lililokuwa na kichwa cha habari
‘MAMA AWAFUNGIA NDANI WANAYE 3 KWA MIAKA 10.’
Habari kutoka Mafia zinasema Muhadia baada ya kufikishwa hospitalini,
alianza kupatiwa matibabu na lishe bora lakini siku hiyo ya kifo chake
(Aprili 15) hali yake ilibadilika ghafla na kuaga dunia saa 1.30
usiku.Marehemu huyo alizikwa Aprili 16, mwaka huu katika Kijiji cha
Kanga kilichopo kilomita 40 kutoka Mafia mjini ambapo gharama zote za
mazishi ziligharamiwa na ofisi ya mkuu wa wilaya.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu juzi, Mkuu wa Wilaya,
Dk.Hamid alisema amesikitishwa na vifo vya ndugu hao wawili waliokufa
kwa mateso makubwa na ya muda mrefu.“Ni bahati mbaya sana ofisi yangu
ilipata taarifa juu ya wagonjwa hao wakiwa katika hali mbaya. Nitoe wito
kwa wananchi kwamba wanapokuwa na matatizo kama hayo wasifiche, watoe
taarifa serikalini ili washughulikiwe mapema,” alisema.
No comments:
Post a Comment