Pages

Friday, November 30, 2012

‘Dada’ aiba mtoto mwenyeji wa mkoa wa Kigoma.

MSAIDIZI wa ndani, Doyi Yusuph (13), mwenyeji wa mkoa wa Kigoma, anasadikiwa kuiba mtoto wa kike, Yasinta Joel (5), katika nyumba aliyokuwa akifanya kazi wilayani Bukombe, Geita, na kisha kutoweka naye kusikojulikana.
Akizungumza  juzi, bibi wa mtoto huyo, Perepatua Alphonce, alisema dada huyo amefanya wizi huo huku akiacha sanduku lake la nguo, jambo ambalo liliwahadaa kwa kutogundua haraka kitendo hicho.

Perepetua maarufu kwa jina na Bibi Mgaya, alisema mjukuu wake huyo alikuwa akisoma chekechea kwa Mwalimu Kapesa na alikuwa akiishi na babu yake, Edward Mgasa.
Alisema dada huyo ambaye alikuwa na wiki moja tangu aanze kazi katika familia ya Mzee Mgasa, alimuiba mtoto huyo Novemba 23, mwaka huu, majira ya saa tatu asubuhi. Wakati akiondoka naye mtoto huyo alikuwa amevaa blauzi ya maua yenye mchanganyiko wa rangi nyekundu na zambarau na sketi ya Jeans rangi ya bluu.

“Niliishaachana na Mzee Mgasa ambaye alioa mke mwingine na walikuwa wakishirikiana kumlea mjukuu wetu. Siku ya tukio mzazi mwenzangu alikuwa kwenye machimbo madogo ya Ng’anzo kwenda kutafuta riziki,” alisema Perepetua.
Alisema amesharipoti suala hilo katika kituo cha polisi cha wilayani Bukombe na kufunguliwa jalada namba USH/IR/177/2012 na kuwaomba raia wema wanaomuona mtoto huyo kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi au kuwasiliana naye kwa simu namba 0755 910 377.

No comments:

Post a Comment