Pages

Friday, November 30, 2012

Poleni tasnia ya sanaa kwa kupoteza wasanii.

Awali ya yote naanza kwa kutoa mkono wa pole kwa wapenda burudani kote nchini kutokana na misiba ya wasanii iliyofuatana, jambo lililoipelekea kuwa na majonzi yasiyokoma.
Awali alianza Maria Khamis ‘Paka Mapepe’ aliyekuwa muimbaji wa muziki wa taarab wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT) aliyefariki kutokana kifafa cha uzazi.
 
Wakati watu wakiwa hawajakaa sawa wala machozi kufutika vema usoni au kwa msemo mwingine naweza kusema ikiwa bado tanga halijaanuliwa sawasawa tasnia ya filamu ikaondokewa na Khalid Mohamed a.k.a Mlopelo (41) aliyeng’ara na kikundi cha Kaole kilichokuwa kikirushwa na kituo cha televisheni cha ITV ambako ndiko alikopata umaarufu wake na hatimaye kushirikishwa katika filamu kadhaa.

Wakati msiba wa Mlopelo haujaisha msanii mwingine wa Bongo Movie John Maganga akafariki Jumamosi iliyopita na kuzikwa Jumanne wiki hii.
Wakati kukiwa kuna msiba wa Maganga Jumatatu usiku msanii Ramadhan Mkiteti alipata ajali maeneo ya Maguzoni Muheza mkoani Tanga.
Hakika wasanii na tasnia wamekumbwa na misiba yote ya uchungu; nachukua fursa hii kuwapa pole.
Ni kweli hakuna msiba unaozoeleka hata siku moja kama babu au bibi yako amefariki miaka kadhaa iliyopita, inauma sana.


Kama hiyo haitoshi hata kwa sisi tuliopoteza wazazi wetu kama mimi ambaye sina mama kwa kweli ninaposikia habari ya msiba huumia sana na kunitonesha machungu ambayo ninayo wakati wote.
Vivyo hivyo napenda kuwapa pole wafiwa hasa mama Mlopelo, Mama Sharo Milionea na wazazi wa Maganga kuwa wamshukuru Mungu kwa yote.

Nikiwa nyumbani kwangu ambapo nilifuatilia kipindi cha ‘Take One’ kinachorushwa na televisheni ya Clouds nilimsikia baba mdogo wa marehemu Maganga aliyejitambulisha kwa jina la Deogratius Shija akibainisha kwamba kifo cha mtoto wao kilitokana na uzembe wa wasoma vipimo X-Ray ambapo wao walipofika katika Hospitali ya Mwananyamala walilazimika kupiga picha ili tatizo libainike.
 
Ndipo iliposomeka kwamba alikuwa na tatizo la kutoboka utumbo hivyo akatakiwa kufanyiwa upasuaji na akafanyiwa upasuaji lakini hali yake haikutengemaa.
Maskini pindi alipopewa uhamisho wa kwenda kutibiwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili (MNH), ambako ndiko kwenye mashine kubwa za kuweza kumsaidia kupumua akiwa huko ndipo akapatiwa vipimo vingine nao wakagundua kwamba bandama lilipasuka hivyo upasuaji aliofanyiwa katika Hospitali ya Mwananyamala ulifanyika kwa makosa.

Kama hiyo haikutosha tabibu bingwa wa magonjwa hayo alikuwa amemaliza muda wake wa kazi hivyo ndugu wakaambiwa wasubiri hadi ambapo angeliingia kazini kesho yake.
Ikumbukwe kwamba wakati huo marehemu Maganga alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine hospitalini hapo.

Lakini hadi tabibu anafika alfajiri hali haikuwa nzuri kwani hata upumuaji wa mgonjwa ulikuwa wa taabu licha ya kusaidiwa na mashine.
Inasikitisha na inauma sana jinsi hali ilivyo na kifo cha Maganga kilivyotokea ni uzembe mtupu.
Jamani mbona hali inatisha kwenye hospitali zetu za serikali? Kwa nini iwe ni wao tu kila mara ni Mwananyamala tu? Hebu wahusika tupieni macho suala hili.

Waangaliwe wasoma vipimo na hata huyo tabibu na jopo lake waseme wazi kama kweli walipomfanyia upasuaji ni kweli walikuta utumbo umetoboka kwani hapa hakuna anayeweza kusema mkweli ni nani. Hivi wizara husika haisikii kadhia zote hizi zinazowakuta wananchi wake?
Nimeguswa na sana na vifo hivi huku kila mmoja akiwa na sababu yake iliyosababisha afe lakini sababu ya Maganga ni uzembe wa baadhi ya matabibu wetu hawakuwa makini kuanzia hatua ya awali.

Huenda wakati mwingine inawezekana ikawa ni uchakavu wa vifaa vya hospitalini kwetu lakini kwa nini iwe hivyo?
Jambo lingine lililonishtua ni kusikia kwamba walishindwa kumwekea mashine ya kupumua kwa sababu iliyopo katika Hospitali ya Mwananyamala haina nguvu hivi ni wagonjwa wangapi wanaopoteza maisha yao hospitalini pale?
Kumbe Mwananyamala kuna siri tena nzito ambayo imefichuliwa na kifo cha Maganga; siri hii ni kumsababishia maumivu makali yaliyosababisha kifo chake, walimkata utumbo pasi na sababu ya kufanya hivyo ilhali ana tatizo lingine na mashine zao hazina nguvu.

Huu ni ukatili kwa baadhi ya watendaji wa serikali kwa kutokuwa makini na kujali wananchi wake ambao wanakufa kwa kulazimishwa kwa matibabu yasiyokidhi na vifaa duni.
Na ni serikali hii hii itakayokaa kimya bila kulitolea ufafanuzi suala hili. Inasikitisha imekuwa ni mazoea sasa kwani historia ya matabibu wasiozingatia weledi inazidi kuandikwa, walipasuliwa wagonjwa kichwa badala ya mguu na mguu badala ya kichwa serikali hiihii ilikaa kimya.
Ndugu wa wagonjwa walishtaki hasa yule aliyepasuliwa kichwa kwani tayari amepewa ulemavu asiokuwa nao.

Vivyo hivyo kama mapenzi ya Mungu yasingetimia kwa kumchukua Maganga ina maana na yeye tayari alikuwa amepewa ulemavu wa utumbo wake na je angeishi vipi katika hali ile endapo yasingemkuta mauti?
Majibu ya hayo yote yanabaki kwa kila mmoja kujitafakari na kuchukua hatua.
Poleni wafiwa wote kwa yote yaliyowakuta; ni mapenzi yake, kila nafsi lazima itaonja mauti sawa lakini mauti nyingine husababishwa na baadhi ya matabibu wasiokuwa makini na kazi zao.
Huu ni mtazamo tu kwenu matabibu na wauguzi wala msiniwekee chuki.

No comments:

Post a Comment