Pages

Friday, March 29, 2013

MASHUJAA BAND WASEMA: CHONDE CHONDE TWANGA, MSTITUCHOKOZE TUTANYOFOA NUSU YA BENDI YENU

KUFUATIA tetesi za baadhi ya wanamuziki wa Mashujaa kutaka kurejea Twanga Pepeta, bendi hiyo ya Mashujaa imepiga mkwara mzito juu ya jambo hilo.

Meneja wa Mashujaa Band, Martin Sospeter ameiambia Saluti5 kuwa anajua Twanga ingependa kurejesha wanamuziki wao wote waliojiunga na Mashujaa lakini amewataka kufanya hivyo kwa umakini mkubwa.
Martin (pichani kushoto) amesema Twanga wahakikishe kuwa wana mikataba na wanamuziki wao kabla gharika halijawaangukia.

“Wao wachukue wanamuziki wetu lakini wajue kuwa kuna siku kisu kitagusa mfupa, hatutavumilia tutazoa wanamuziki wao wote ambao hawana mikataba, tutanyofoa zaidi ya nusu ya bendi kuanzia mstari wa nyuma kwa wapiga vyombo hadi mbele kwa waimbaji.

“Tena tutafanya hivyo Ijumaa kuamkia Jumamosi, dansi lao la Mango Garden halitalia, hatutanii kwenye hili, kama wanachukua wanamuziki wetu basi wahakikishe kuwa wanamuziki wao wote wana mikataba, vinginevyo wasitulamu,” alisema Martin ambaye nae alitokea Twanga Pepeta.
Miongoni mwa wanamuziki wanaohusishwa kurejea Twanga Pepeta ni MCD, Lilia Internet na Chaz Baba huku mpiga solo Amos aliyewahi kuitumikia moja ya bendi za ASET akiwa tayari ameshanyakuliwa na Twanga Pepeta.

No comments:

Post a Comment