Pages

Friday, March 29, 2013

Mtoto mgonjwa atelekezwa Kivukoni

MWANAMKE asiyefahamika juzi alimtelekeza mtoto mdogo wa kike anayekadiriwa kuwa na miaka mitano ambaye ni mgonjwa katika eneo la Kivuko cha Kisorya, wilayani Bunda, Mara.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kisorya, Mashaka Mahulilo, alisema mtoto huyo ambaye pia amepooza mguu mmoja alitelekezwa juzi, majira ya saa 9:30 mchana katika eneo la kijiji cha 

Kisoya, baada ya Kivuko cha MV Ujenzi kinachofanya safari kati ya ng’ambo ya Kisorya, wilayani Bunda, na Ngoma Lugezi wilayani Ukerewe kutia nanga katika eneo hilo.

Alisema mwanamke huyo alikuwa ni kati ya abiria waliokuwa ndani ya kivuko hicho wakitokea wilayani Ukerewe na kwamba baada ya kufika eneo hilo alimtelekeza mtoto huyo.
Mahulilo alisema mtoto huyo ambaye ni kiziwi aliachwa na mama yake eneo hilo, akiwa na mifuko miwili midogo ya nailoni iliyokuwa na nguo zake.

Alisema mtoto huyo aliokotwa na wasamaria wema akiwa ukingoni mwa daraja la kivuko hicho na kwamba alichukuliwa na mwananchi mmoja mkazi wa kijiji hicho aliyekabidhiwa mbele ya viongozi wa serikali ambaye sasa ndiye anayeishi naye.
Kutokana na tukio hilo, baadhi ya wananchi wamelaani kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo.

No comments:

Post a Comment